Rais Samia afunguka mazito Mkutano wa wakuu wa nchi Afrika atoa msisitizo

 

Rais Samia Suluhu Hassan kupitia ukurasa wake mtandao wa twita ametoa ufafanuzi kuhusu ushiriki wa Tanzania katika mjadala baina ya viongozi na wakuu wa nchi za Afrika kuhusu maendeleo ya rasilimali watu.


Katika majumuisho yake Rais Samia ameandika “Juma hili tumekuwa na mkutano na mjadala muhimu baina ya viongozi na wakuu wa nchi za Afrika kwa maendeleo na mustakabali wa nchi zetu na Bara letu, kuhusu Maendeleo ya Rasilimali Watu”


Ninamshukuru sana Mwenyezi Mungu kwa kuijalia nchi yetu fursa hii adhimu ya kukutanisha viongozi hawa katika nchi yetu kwa jambo hili lenye kheri na muhimu kwa maendeleo yetu.


Mkutano huu umebeba kaulimbiu ya “Kuchochea Ukuaji wa Uchumi Afrika: Kuongeza Uzalishaji wa Vijana kupitia Mafunzo na Ujuzi’’, ajenda ambayo ndio moyo wa mataifa yetu – uwekezaji katika rasilimali watu, hususani vijana. 


Mbali na kufikia azimio la pamoja (Azimio la Dar es Salaam) ambalo pamoja na mambo mengine litakuza ushirikiano wetu katika uwekezaji na maendeleo ya rasilimali watu, tumeshirikishana yale yanayofanyika katika nchi zetu. 


Sisi Tanzania tunaamini katika falsafa za waasisi wetu kuhusu umuhimu wa uwekezaji katika rasilimali watu ili kuleta maendeleo na uhuru wa kweli. Falsafa hizi bado zinaishi na ni sehemu ya dira yetu katika utendaji. Baba wa Taifa Hayati Mwalimu Julius Nyerere aliwahi kusema, “Maendeleo ni watu. Watu ndio walengwa, waanzilishi na wanufaika wa chochote kinachoitwa maendeleo.”



Tumeshirikisha uzoefu wa nchi yetu na safari yetu katika kukuza rasilimali watu kuanzia mimba inapotungwa hadi mwananchi anapofikia umri wa kutoa mchango wake kwa maendeleo ya Taifa. Pamoja na mambo mengine, tumeshirikishana uzoefu katika mambo tisa ambayo serikali inafanya katika eneo hili: 


1. Kutenga fedha kwa ajili ya afua mbalimbali za lishe na huduma za Afya ya Uzazi wa Mama na Mtoto. 


2. Kuanzisha vituo vya elimu ya awali (tunaendelea na ujenzi wa shule za awali katika kila shule ya msingi nchini). 


3. Mapitio na maboresho ya Sera ya Elimu, mitaala na programu za mafunzo ili ziendane na mazingira pamoja na mahitaji ya sasa ya maendeleo.


4. Uanzishwaji wa Mfuko wa Kusaidia Kaya Masikini, ujulikanao kama Tanzania Social Action Fund (TASAF). Lengo likiwa kupunguza umaskini na kuboresha upatikanaji wa huduma za afya na

elimu. Tangu mwaka 2000, zaidi ya kaya milioni moja zimenufaika. 


5. Uanzishwaji wa Programu ya elimu bila malipo kwenye ngazi za elimu ya awali, elimu ya msingi na sekondari kuanzia Kidato cha Kwanza hadi cha sita.


6. Uwekezaji kwenye elimu ya ufundi na mafunzo ya amali, ikiwa ni pamoja na kutoa ujuzi bobezi ili kuongeza tija, ushindani na uwezo wa ndani katika kutumia maliasili za nchi yetu. Sasa tunajenga chuo cha VETA katika kila Wilaya nchini. 


7. Kuwezesha vijana kiuchumi kupitia mikopo inayotolewa na Halmashauri kwa Vijana.


8. Kuruhusu Watoto walioachwa masomo hasa wa kike waliopata mimba kuweza kurejea masomoni. 


9.  Kupitia Wizara ya Kilimo Serikali, inatekeleza Programu ya kuwezesha ushiriki wa vijana katika Kilimo Biashara (Building a Better Tomorrow Youth Initiative for Agribusiness (BBT-YIA). Programu hii inatarajiwa kuongeza ajira kwa vijana kufikia milioni 3 na kuongeza ukuaji wa sekta ya Kilimo hadi kufikia asilimia 10 ifikapo 2030 (Ajenda 10/30).

Chapisha Maoni

0 Maoni