Mh. Mchengerwa azindua Kamati ya Ushauri ya ugawaji wa vitalu vya uwindaji

Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Mohamed Mchengerwa amezindua Kamati ya Ushauri ya Ugawaji wa Vitalu vya Uwindaji wa Kitalii nchini   huku akiitaka kurekebisha kasoro zote zilizojitokeza siku za nyuma huku akitaka ugawaji ufanyike kwa uwazi ili kuendana na wakati wa sasa hatimaye tasnia hiyo ichangie kwa kiwango stahiki kwenye uchumi wa taifa.

Akisoma hotuba yake wakati wa uzinduzi leo Julai 11, 2023 jijini Arusha, Waziri Mchengerwa amesema ameiunda kamati hiyo kwa mamlaka aliyopewa kwa mujibu wa kifungu cha 38 (1) na (2) ya Sheria ya Uhifadhi wa Wanyamapori sura ya 283 huku akisisitiza kwamba   Kamati hiyo inatakiwa kuboresha changamoto zote ili tasnia ijiendeshe kibiashara na kupunguza urasimu na mikinzano isiyokuwa na tija kwa Taifa.

“Ni imani yangu kwamba, kwa kuzingatia ushauri utakaotolewa na Kamati hii tasnia ya Uwindaji wa Kitalii itazidi kuimarika na kuvutia wawekezaji wa ndani na nje ya Nchi. Pia Kamati itasaidia kuhakikisha vitalu vyote vinapata wawekezaji ili kuongezea mapato ya Serikali ikiwa ni pamoja na vitalu 43 ambavyo kwa sasa vipo wazi.” Amesisistiza, Mhe. Mchengerwa

Aidha, amesema anatarajia Kamati hiyo itafanya kazi kwa ufanisi na weledi katika utendaji kwa kuzingatia kuwa imesheheni wataalamu kutoka katika nyanja mbalimbali.

Amefafanua kuwa uwindaji wa kitalii unachangia katika pato la Taifa hususani fedha za kigeni na kwamba kwa wastani, Serikali inakusanya takriban shilingi Bilioni 30 kwa mwaka kutokana na Uwindaji wa huo na unachangia ajira za rasmi na zisizo rasmi kwa jamii.

Amesema kiasi hicho ni kidogo ukilinganisha na utajiri wa raslimali za wanyamapori hapa nchini ambapo ameitaka Kamati hiyo  kufanya kazi na kujiwekea malengo  makubwa zaidi.

Aidha, ameitaka Kamati hiyo kuzitambua  changamoto zinazokabili tasnia hiyo ili kuja na mikakati ambayo itasaidia kuboresha  sekta  hiyo.

Amezitaja baadhi ya changamoto hizo kuwa ni pamoja na  mabadiliko ya Sera na Sheria za  Mataifa yanayoleta watalii wengi wa uwindaji, mabadiliko ya tabia nchi,uvamizi wa mifugo katika vitalu vya uwindaji wa kitalii hivyo kuathiri ustawi wa tasnia hii, na kampeni za wapingaji wa uwindaji wa kitalii ambazo kwa kiasi kikubwa zimeingilia maamuzi ya Mkataba wa Kimataifa unaosimamia Biashara ya Wanyamapori na Mimea iliyopo Hatarini kutoweka (CITES).

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Kamati ya Ushauri wa Ugawaji Vitalu

Profesa Jafary Kideghesho, amemhakikishia Waziri Mchengerwa  kuwa Kamati yake itafanya kazi kwa weledi ili kufikia  maono na Serikali ya kutaka tasnia  hiyo  kuchangia  katia uchumi.

Naye Katibu wa Kamati hiyo ambaye pia ni Kamishna wa Mamlaka ya Wanyamapori nchini (TAWA) Mabula Nyanda amemshukuru Mhe. Mchengerwa  kwa kuiunda Kamati  hiyo ambapo amesema  itasaidia kuboresha  tasnia hiyo kwa kuwa imejumuisha  wataalaam waliobobea  katika tasnia hiyo.

Mara baada ya uzinduzi huo waziri Mchengerwa ametoa  nyaraka  na miongozo mbalimbali kwa wajumbe wote ikiwa ni  namna ya kuwakabidhi nyenzo kwa ajili ya utekelezaji wa  kazi zao.

Na John Mapepele

Chapisha Maoni

0 Maoni