Mh. Majaliwa ashuhudia gwaride maalum la Jeshi la Wanamaji la Urusi

 

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amekuwa miongoni mwa Wakuu wa Nchi na Serikali waliohudhuria Maonesho ya Gwaride Maalum la Jeshi la Wanamaji la Urusi yaliyofanyika jana Senatskaya Marina, St. Petersburg, Urusi.

Viongozi hao ni wale walioshiriki Mkutano wa Pili wa Kilele baina ya Wakuu wa Nchi na Serikali kutoka mataifa ya Afrika na Urusi Jijini St. Petersburg, Urusi ambako yeye alimwakilisha Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan.

Maonesho hayo yamefanyika ikiwa ni siku ya Jeshi la Wanamaji la Urusi na maadhimisho ya kukumbuka kuanzishwa kwa jeshi hilo ambayo hufanyika Julai 30, kila mwaka.

Katika maonesho hayo Rais wa Urusi, Vladmir Putin alipita kwenye boti maalum akiwasalimia wananchi waliojipanga kwenye kingo za mto Bolshaya Neva na kupokea salamu za kijeshi. Alipomaliza akavushwa na boti ndogo kwenda kwenye jukwaa maluum na kuhutubia Taifa.

Baada ya hapo meli na boti za kivita zilipita mbele ya jukwaa kuu na kutoa heshima. Kisha akaenda kuwasalimia mmoja baada ya mwingine viongozi wa Afrika waliohudhuria maonesho hayo na baadaye alipanda nao kwenye boti hiyo maalum.

Chanzo: Ofisi ya Waziri Mkuu

Chapisha Maoni

0 Maoni