Watu kadhaa wamezama majini jana maeneo ya kisiwa cha Jugu
baada ya mitumbwi miwili midogo waliyokuwa wakisafiria kuzidiwa uzito na kuzama
katika ziwa Victoria, ambapo inaarifiwa kuwa bado uopoaji haujaanza kwa
kukosekana wataalamu, wazamiaji na vyombo vya uopoaji.
Taarifa zilizonifikia kutoka kijiji cha Buromba,
Mwibara-Bunda, mkoani Mara, zinasema katika tukio hilo, zaidi ya watu 15, wengi
wao wakidaiwa kuwa ni watoto, bado wapo ndani ya maji tangu jana saa 10:00
jioni walipozama, hali inayohofiwa kwamba tayari watakuwa wamekufa.
Tayari watu 12 waliokolewa, wamelazwa katika Hospitali ya
Misheni, Kibara japo hali zao zinaelezwa kuwa si nzuri.
Imeelezwa kwamba, watu hao, washiriki wa Kanisa la Last
Church, waliokuwa wakitoka kusali kijiji jirani cha Mchigondo, mtumbwi wa nyuma
ulinyunyuka (Ulitoboka) na kuzama, mtumbwi wa mbele ulirudi kuwaokoa, ulipofika
eneo la tukio, watu wote waliung'ang'ania kutaka kupanda, nao wakauzamisha.
Eneo hilo la tukio inaelezwa kuna mkondo mkubwa wa maji,
wenye mwelekeo wa Majita, hivyo huenda miili ya watu hao wanaohofiwa kufa
ikasombwa na mkondo huo wa maji kupelekwa mbali zaidi.
Taarifa zinadai kwamba, asubuhi hii, wananchi watajikusanya
kuangalia namna ya kufanya, kwa vifaa hafifu kujaribu kuiopoa miili ya watu
hao.
Kamanda wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Mkoa wa Mara,
Agostino Magere amethibitisha kutokea kwa tukio hilo na kuahidi kutoa taarifa
zaidi baadaye.
Na. Masau Kuliga Bwire
0 Maoni