Waziri Mkuu Kassim Majaliwa ametoa rai kwa wafanyabishara
nchini kutumia maonesho ya kibiashara ya kimataifa ya Sabasaba sambamba na
fursa za makampuni ya kigeni ili kujifunza na kujipanga kuhudumia masoko
makubwa ya ndani, kikanda na kimataifa.
Amesema kufunguka kwa
Soko la Eneo Huru la Afrika – AfCFTA ambalo linakadiriwa kuwa na walaji zaidi
ya bilioni 1.3 kutoka nchi 53 barani Afrika ni fursa kubwa kwa wafanyabiashara
wa Tanzania.
"niwaombe wale wote wenye bidhaa zenye viwango na
wanaoweza kukidhi vigezo kujisajili kupitia Wizara ya Uwekezaji, Viwanda na
Biashara ili kunufaika na mpango huo. Ni muhimu sana tukaweka jitihada za dhati
kuyafikia masoko haya na siyo kuwa waangaliaji tu na kulalamika."
Ameyasema hayo jana, Julai 05, 2023 alipomwakilisha
Mheshimiwa Dkt. Rais Samia Suluhu Hassan katika ufunguzi wa maonesho ya
biashara ya kimataifa ya 47, Temeke Dar es Salaam.
Aidha, amezitaka Wizara ya Uwekezaji, Viwanda na Biashara
ishirikiane na Wizara ya Kilimo katika kuandaa mpango wa pamoja kuhakikisha
uzalishaji unafanyika kwa kuzingatia mahitaji ya masoko ya ndani na nje ya
nchi.
"Wizara hizi mbili lazima zisomane kiutendaji. Aidha,
wataalam wa TanTrade washirikishwe kikamilifu katika kutekeleza majukumu ya
utafutaji na ufunguaji wa fursa za masoko ndani na nje ya nchi."
Mheshimiwa Majaliwa ameipongeza. TanTrade kwa kutenga eneo
maalum kwa ajili ya Wamachinga ili na wao wajifunze mbinu za kukua kibiashara.
"Niwasihi wamachinga jifunzeni vizuri teknolojia na
mbinu za ufanyaji biashara muweze kukua zaidi.
Amesema ni azma ya Serikali ya Awamu ya Sita kutengeneza
mabilionea kupitia Biashara. Pia, ni fahari kubwa kwa nchi kuona wamachinga
wanakua na kufanya biashara kimataifa.
Katika hatua nyingine Mheshimiwa Majaliwa amezitaka Halmashauri zote nchini kuweka utaratibu wa kuwapanga wamachinga katika maeneo rafiki ya kibiashara, ili wafanye biashara zao kwa uhuru na kuchangia uchumi.
Amesema ni vyema sasa maeneo ya wamachinga yawekewe
miundombinu yote muhimu ili kuliinua kundi hilo kutoka wafanyabiashara wadogo
kuelekea wakati na hatimaye wakubwa.
Akizungumza kabla ya kumkaribisha Mgeni Rasmi, Waziri wa
Viwanda na Biashara wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar amesema Wizara zote
zitaendelea kushirikiana na kuratibu fursa za wafanyabiashara nchini ili kukuza
uchumi.
Awali Naibu Waziri Uwekezaji na Viwanda, Exaud Kigahe amesema
Maonesho hayo ni nyenzo muhimu katika kuwakutanisha wafanyabiashara kutoka
ndani na nje ya nchi na kuwapa nafasi ya kutengeneza mitandao ya kubiashara
pamoja na kupata masoko ya bidhaa na huduma wanazozizalisha.
Naye Mwenyekiti wa Bodi ya Tantrade, Olingeta Mbamba amesema
Mamlaka hiyo pamoja na mambo mengine imefanikiwa kushirikiana na Ofisi za
Balozi katika nchi za Kenya na Malawi kuratibu wafanyabiashara 206 kutoka
Tanzania katika misafara ya kibiashara katika nchi za Sudani Kusini na Malawi
ambayo imeweza kutangaza fursa kwa wafanyabiashara wa Tanzania.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Maendeleo ya
Biashara Tanzania (Tantrade ) Bi Latifa Mohamed amesema Tantrade ndio yenye
jukumu la kukuza na kuendeleza biashara
Nchini.
"Tantrade inafanya shughuli mbalimbali ikiwemo kufanya
utafiti wa masoko wa bidhaa zinazowasilishwa nchini, kutoa taarifa za biashara,
kuzijengea uwezo Jumuia za wafanyabiashara juu ya namna bora ya kusimamia
shughuli za biashara ndani na nje ya nchi".
Mwisho
0 Maoni