Bodi ya Wakurugenzi wa Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori
Tanzania (TAWA) imezindua mradi mkubwa wa maji unaogharimu shillingi Millioni
400 katika Kijiji cha Nkonko kilichopo kata ya Nkonko Wilaya ya Manyoni Mkoani
Singida
Mradi huo unaoelezwa kuzalisha Lita 2,000 za maji Kwa saa
na kutarajiwa kuwanufaisha wananchi
zaidi ya 8,000 na taasisi mbalimbali za Serikali ikiwemo shule ya Sekondari
yenye jumla ya wanafunzi 200 na walimu 14 umezinduliwa leo Julai 5, 2023 na Mwenyekiti
wa Bodi ya Wakurugenzi wa TAWA Mej. Jen. (Mstaafu) Hamis Semfuko
Akizungumza katika hafla ya Uzinduzi wa mradi huo, Mwenyekiti
huyo amesema TAWA imeamua kuunga mkono juhudi za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan katika kutatua tatizo la miundombinu ya
maji linalowakabili wananchi.
"Sisi TAWA tumeamua kuunga mkono juhudi za Mhe. Rais
katika kutatua tatizo hili kubwa la maji hapa nchini, tumefanya hivyo Kwa
vitendo kama mnavyoona hapa na maeneo mengine lakini vilevile tumefanya hivyo
Kwa kununua gari letu wenyewe la kuchimba maji" amesema
Mej. Jen. (Mstaafu) Semfuko amesisitiza kuwa TAWA chini ya Serikali ya Rais Samia
imedhamiria kupunguza changamoto Kwa wananchi katika maeneo yote yaliyo katika
usimamizi wao
"Moja ya tatizo la Taifa letu ni miundombinu ya maji na
ndio maana TAWA katika maeneo yote tutakayokaa tutahakikisha kwamba tunatoa
huduma hiyo Kwa wananchi " amesisitiza
Akitoa shukrani zake Kwa niaba ya wananchi, diwani wa kata ya
Nkonko Mhe. Ezekiel Ezekiel amesema wananchi wanajivunia uwepo wa TAWA katika
eneo lao kwani kupitia taasisi hiyo wamepata manufaa makubwa ikiwemo mradi
mkubwa wa maji, kukamilishwa Kwa ujenzi wa hosteli ya wasichana katika shule ya
Sekondari kutokana na asilimia 20 ya fedha wanazopata kupitia shughuli za
Uwindaji wa Kitalii unaofanywa maeneo hayo na msaada wa haraka wanapovamiwa na
wanyama Wakali na Waharibifu
Sambamba na Uzinduzi wa mradi huo, bodi ya Wakurugenzi wa TAWA ilitembelea na
kukagua mradi wa barabara yenye urefu wa Kilometa 142 inayotengenezwa ndani ya
Pori la Akiba Kizigo Kwa mashirikiano kati ya TAWA na Wadau wa Uhifadhi WCS na EBN pamoja na kupokea jumla
ya viti 10 vya walemavu vyenye thamani ya shillingi 8,000,000/= (Millioni Nane)
kutoka Kwa mwekezaji Nicolas Negre wa EBN Hunting Safari Ltd
Naye Kamishna wa Uhifadhi wa TAWA Mabula Misungwi Nyanda,
amewapongeza Wadau wa Uhifadhi WCS na EBN Kwa ushirikiano mkubwa wanaoutoa Kwa
Taasisi anayoisimamia (TAWA) unaofanikisha shughuli za ulinzi na Uhifadhi
katika Pori la Akiba kizigo na kuwasihi waendeleze mashirikiano hayo Kwa
mustakabali wa Pori hilo na Uhifadhi Kwa ujumla Nchini.
Pia amempongeza Kamanda wa Pori hilo, Oggosy Gasaya Kwa kazi
nzuri anayoifanya na Kwa ushirikiano mzuri anaoutoa Kwa wananchi wanaozunguka
Pori hilo pamoja na Wadau wa uhifadhi
Na Beatus Maganja - SINGIDA
0 Maoni