WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amewataka wanadiaspora wa
Tanzania wazingatie sheria za nchi wanazoishi ili waendelee kutunza heshima ya
nchi yao.
Ametoa wito huo wakati akizungumza na Watanzania waishio St.
Petersburg, Urusi ambako alimwakilisha Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwenye
Mkutano wa Pili wa Kilele baina ya Wakuu wa Nchi na Serikali kutoka mataifa ya
Afrika na Urusi.
“Baadhi yenu mko hapa mnatafuta fursa, na wengine wengi wako
hapa kwa masomo. Zingatieni sheria za nchi hii, tunzeni heshima ya Tanzania.
Teteeni Taifa la Tanzania, zungumzieni fursa zilizopo nyumbani,” alisema Waziri
Mkuu
Akisisitiza umuhimu wa kukitangaza Kiswahili, Waziri Mkuu
alisema: “Kiswahili kiendelee kutangazwa kwa bidii kwani Kiswahili ni fursa na
Kiswahili ni ajira. Tukitangaze Kiswahili na tushike nafasi za kutangaza lugha
yetu kwa kasi kwa sababu tuna historia ya muda mrefu na Urusi ambao wamekuwa wakitumia
lugha hii,” alisema.
Alisema katika baadhi ya vikao vyake na wawekezaji wa
Kirusi, hakupata shida ya mkalimani kwa sababu walikuwa na mtu wao ambaye
anatafsiri moja kwa moja kutoka Kirusi kwenda Kiswahili na Kiswahili kwenda
Kirusi. “Lakini na sisi ubalozini kwetu tuna Afisa Uchumi ambaye alitusaidia
kutafsiri Kiswahili kwenda Kirusi kwenye baadhi ya vikao. Tena aliongea kwa
ufasaha zaidi. Tusiache fursa hii itupite,” aliwasisitiza.
Waziri Mkuu alitumia fursa hiyo kuwapa picha halisi ya maendeleo
na kiuchumi yanayofanyika nchini chini ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu
Hassan zikiwemo sekta za elimu, afya, miundombinu, utalii, kilimo, maji na
akawahakikishia kwamba Tanzania iko salama, wao waweke bidii kwenye masomo yao.
Mapema, akimkaribisha Waziri Mkuu kuzungumza na washiriki wa
kikao hicho, Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki,
Balozi Mbarouk Mbarouk alisema mbali na kazi ya kudumisha mahusiano ya kirafiki
na kidiplomasia kati ya Tanzania na nchi nyingine, Serikali imeendelea kuratibu
masuala ya Diaspora.
“Hivi sasa, wizara imekamilisha Mapitio ya Sera ya Mambo ya
Nje ya Mwaka 2001, ambayo inajumuisha masuala ya Diaspora. Ili kuondokana na
tatizo la ukosefu wa takwimu sahihi za idadi ya Diaspora wetu kote ulimwenguni,
tarehe 22 Mei, 2023 Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki,
Dkt. Stergomena Tax alizindua rasmi Mfumo wa Kuwasajili Diaspora Kidigitali.
Mfumo huo, uliotengenezwa na Wataalam Wazawa utasaidia kurahisisha usajili wa
Diaspora wenye asili ya Tanzania pamoja na wanafunzi.”
“Ni dhahiri kuwa Diaspora waliopo katika eneo zima la
uwakilishi wa ubalozi wetu hapa Urusi, sasa hawatalazimika tena kusafiri kwenda
ubalozini Moscow ili kujisajili. Napenda kutumia fursa hii kuwahamasisha
Diaspora wote wajisajili kwa wingi.”
Alisema ana imani kuwa takwimu zitakazopatikana kupitia
mfumo huo, zitaiwezesha Serikali kupanga na kuandaa kwa usahihi mahitaji
yanayohitajika ili kuwapatia Diaspora huduma wanazozihitaji, ikiwemo huduma za
kibenki, Hati za Kusafiria, Vitambulisho vya Taifa na vitambulisho rasmi vya
utambuzi wa diaspora wakati wa utekelezaji wa Hadhi Maalum.
“Hadi sasa, mfumo huu umetuwezesha kufahamu kuwa tunao
diaspora wenye asili ya Tanzania katika nchi za Vanuatu, Albania, Antigua na
Barbuda, Kazakhstan, Azerbaijan pamoja na America Samoa ambazo nchi yetu haina
uwakilishi wa Kibalozi,” alisema.
Akisoma risala yao, Mwenyekiti wa Diaspora katika Shirikisho
la Urusi na Nchi huru za Jumuiya ya Madola (CIS), Pascal Gura alisema jumuiya
yao (TADRU- CIS), ina wanachama zaidi ya 200 walioko sehemu tofauti za nchi
hiyo.
Alisema kwa sasa wanadiaspora hao wanakabiliwa na changamoto
ya mifumo ya kifedha kutokana na vikwazo vya kiuchumi. “Changamoto hii
inatokana na Shirikisho la Urusi kuondolewa katika mfumo wa uhamishaji fedha
(Swift) ambao unatumiwa na mabenki kupitia kadi za ‘‘Visa na Master card’’.
“Kwa sasa kadi pekee zinazokubali katika baadhi ya mabenki
katika Shirikisho la Urusi ni kadi zinazotumia mfumo wa Union Pay. Hivyo,
tunaomba benki za Kitanzania zipanue wigo kwa kutoa kadi zenye mfumo wa Union
Pay kwa kuwa itaimarisha pia fursa za kibiashara kati ya Tanzania na Urusi,”
alisema.
Wanadiaspora hao pia walimkabidhi Waziri Mkuu tuzo ya Rais
Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kutambua juhudi zake katika kuwaletea wananchi
maendeleo.
Mkutano huo ulihudhuriwa na Waziri wa Habari, Utamaduni na
Michezo wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar Tabia Maulid Mwita, Naibu Waziri wa
Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Mbarouk Mbarouk, Naibu
wa Waziri wa Fedha na Mipango wa SMZ, Ally Suleiman Ameir, Balozi wa Tanzania
nchini Urusi, Balozi Fredrick Kibuta na watendaji wengine wa Serikali.
Chanzo: Ofisi ya Waziri Mkuu
0 Maoni