WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema Serikali itahakikisha kuwa mikataba ya utekelezaji wa makubaliano ya uendeshaji wa maeneo ya bandari nchini kati ya Serikali ya Tanzania na Serikali ya Dubai kupitia Kampuni ya DP World itazingatia maslahi ya nchi na kuleta manufaa kwa Taifa letu.
Waziri Mkuu
ameyasema hayo leo (Jumatano, Juni 28, 2023) wakati akitoa hoja ya kuahirisha
Mkutano wa 11 wa Bunge la 12 la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ambapo
amesisitiza kuwa makubaliano yaliyoingiwa yanalenga kuweka msingi wa
ushirikiano baina ya Serikali ya Tanzania na Serikali ya Dubai.
Mheshimiwa
Majaliwa amesema kwa kuwa bandari ya Dar es salaam ndiyo kitovu cha huduma za
bandari nchini Serikali iliamua kutafuta Kampuni yenye uwezo na uzoefu mkubwa
katika uendeshaji wa bandari duniani kwa teknolojia za kisasa ili kuiwezesha
bandari hiyo kufanya kazi kwa ufanisi, kuongeza mapato ya nchi na kuchagiza
sekta nyingine za kiuchumi.
Amesema
Serikali za Tanzania na Dubai zimeingia makubaliano kwa lengo la kuanzisha ushirikiano
wa kiuchumi na wa kijamii katika uendeshaji wa maeneo ya bandari nchini kupitia
Kampuni ya DP World, ambayo imeonesha kuwa na utaalamu, uwezo na uzoefu mkubwa
katika uendeshaji wa bandari 190 katika nchi 68 barani Afrika, Asia, Ulaya,
Amerika ya Kaskazini na Kusini.
“Kuhusu umiliki wa bandari, nilihakikishie
bunge lako na wananchi kwa ujumla kwamba, kupitia Sheria ya Bandari ya Mwaka,
2004, Mamlaka ya Bandari Tanzania imekasimiwa haki ya kuwa mmiliki wa maeneo
yote ya bandari nchini na haina uwezo wa kutoa umiliki huo kwa kampuni
nyingine. Haki iliyopewa kwa mujibu wa sheria hiyo ni kuingia mikataba ya
ushirikiano wa kupangisha na kuruhusu sekta binafsi kuendesha sehemu ya maeneo
hayo.”
Waziri Mkuu
amesema wakati wote wa utekelezaji wa makubaliano hayo na mikataba
itakayoingiwa, vyombo vya ulinzi na usalama vitaendelea kutekeleza majukumu yao
katika eneo la mradi kama vilivyofanya katika kipindi cha miaka yote 22 ya
mkataba na mwekezaji wa awali (TICTS) aliyemaliza mkataba wake. “Kuhusu mapato,
ninapenda kuwahakikishia Watanzania kuwa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA)
itaendelea kusimamia masuala ya mapato ya Serikali kutoka kwa mwekezaji kwa
mujibu wa sheria na mkataba.
Hata hivyo,
Waziri Mkuu amesema Serikali itaendelea kupokea mapendekezo, maoni na ushauri
kutoka kwa waheshimiwa wabunge, wananchi na wadau mbalimbali. “Kwa msingi huo,
niielekeze Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi iendelee kuratibu utoaji wa elimu na
ufafanuzi wa hoja za wananchi.
“Nitumie
fursa kutoa rai kwa Watanzania wenzangu tusiruhusu mgawanyiko wa aina yoyote
ile tunapotoa maoni yetu kuhusu uwekezaji wa bandari, tuepuke kujadili itikadi
za kisasa, udini, ukabila, ukanda au vyovyote vile, muhimu tuenzi tunu yetu ya
amani na mshikamano wa Taifa letu iliyojengwa na waasisi wetu.”
Amesema
Juni10, 2023 Bunge lilipata fursa ya kuchangia, kuishauri Serikali na kupitisha
azimio la mapendekezo ya kuridhia makubaliano baina ya Serikali ya Tanzania na
Serikali ya Dubai kuhusu ushirikiano wa kiuchumi na kijamii kwa ajili ya
uendelezaji na uboreshaji wa utendaji kazi wa bandari nchini, hivyo
amewapongeza wabunge wote kwa michango yao na kwa kuona umuhimu na tija katika
jambo hilo na kuamua kulipitisha azimio hilo.
0 Maoni