Serikali yaweka mkono mrefu kwenye vyama vya ushirika


Naibu Waziri wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi Mhe. David Silinde amevitaka vyama vya ushirika kujisajili katika mfumo na kupatiwa leseni ikiwa ni pamoja na Vijana na wanawake kujiunga ili waweze kujikwamua kiuchumi.

Naibu Waziri Silinde ametoa wito huo mkoani Tabora kwa niaba ya Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Hamis Ulega wakati wa Ufunguzi wa Maadhimisho ya Siku ya Ushirika duniani(SUD) .

Amesema Serikali  imedhamiria kuimarisha na kuendeleza azma yake ya kuimarisha, kusimamia na kuendeleza Sekta ya Ushirika nchini kwa lengo la kuondoa umaskini na kujenga uchumi imara wa Wananchi.

Silinde amelitaka Shirika  la ukaguzi wa vyama vya ushirika (COASCO)kuendelea kuimarisha mifumo ya udhibiti na usimamizi wa mali ikiwemo fedha za vyama hivyo.


Aidha ametoa wito kwa Chuo cha Ushirika kuendelea kutoa elimu ya ushirika kwani bado wananchi wengi hawana uelewa na umuhimu wa kujiunga na ushirika ikiwa ni pamoja na shirikisho la vyama vya ushirika kutoa huduma kwa vyama hivyo kwenye mafunzo, masoko, utafiti na ushauri wa namna bora ya kuendesha vyama hivyo.


“Serikali ina azma ya kuimarisha Ushirika kutokana na jitihada mbalimbali zinazoendelea ikiwemo kuimarisha na kukamilisha kanzidata na kusajili  Wakulima nchini ili taarifa hizo ziweze kusaidia katika usimamizi wa Vyama vya Ushirika, usambazaji wa pembejeo na Viwatilifu kwa lengo la kuongeza uzalishaji na hatimaye kukuza masoko kupitia Ushirika” amesema 


Kwa upande wake Makamu Mwenyekiti wa Tume ya Maendeleo ya Ushirika Irene Madeje kwa niaba ya Mwenyekiti wa Kamisheni Abdulmajid Nsekela amesema miongoni mwa vipaumbele vya kuimarisha Ushirika vya Tume ni pamoja na kuimarisha matumizi ya Mifumo ya TEHAMA katika usimamizi na uendeshaji wa Vyama hasa kupitia Mfumo wa Usimamizi wa Vyama vya Ushirika unaosimamiwa na Tume.

Amesema mpango uliopo ni kuibadilisha Benki ya Ushirika ya KCBL kubadilka kuwa Benki ya Ushirika ya taifa (NCBL) 

“Napenda kuvisisitiza vyama vya ushirika pamoja na watu binafsi na makampuni kuendelea kununua hisa katika benki ya ushirika ili kuwezesha benki ya Ushirika kuanza kwa wakati” 

Madeje amesema ipo haja ya kuangalia sera sheria na kanuni za usimamizi wa vyama vya ushirika ili kuanisha changamoto mbalimbali za kisera ili kutoa nafasi kwa vijana kushiriki kikamilifu katika ushirika ili uweze kuwa endelevu.

Amesema mkakati mwingine wa tume hiyo ni pamoja na kuvijengea vyama vya ushirika viweze kujfanya utambuzi wa mali na kuzirasimisha ili kuziendeleza kufanya uwekezaji ili mali hizo ziweze kuzalisha na kuleta tija na manufaa kwa wanaushirika.

Kwa upande wake Mrajisi wa vyama vya ushirika Tanzania Dk Benson Ndiege amesema hali  ya ushirika nchini Tanzania imeendelea kukua ambapo Vyama 7,300 vimeandikishwa na wanachama 8,000 wananchi wanaopata huduma ni zaidi ya mara tatu.



Akizungumzia umuhimu wa maadhimisho hayo ambayo kilele chake ni Julai mosi amesema  yatasaidia kuwaunganisha wanaushirika na wabia wa maendeleo ili kuimarisha mahusiano,kuwakutanisha wadau wa ushirika na wadau na viongozi wa serikali.



Faida nyingine ni Kutangaza kazi za wanaushirika na kuhabarisha umma juu ya falsafa za ushirika na Kujadili changamoto wanazopitia katika vyama vya ushirika na mikakati ya kuboresha 


Chapisha Maoni

0 Maoni