Kifo tata mwanafunzi UDOM chaiibua THBUB

 

Tume  ya haki za Binadamu na Utawala Bora (THBUB) Imetangaza kuanza rasmi  uchuguzi  wa  kifo cha mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM) Nusura  Hassan Abdallah, aliyedaiwa kufariki akiwa anapatiwa matibabu  katika hospitali ya Faraja Mkoani Kilimanjaro.


Akizungumza leo Mei 10 jijini  Dodoma Mwenyekiti wa Tume Hiyo Jaji Mstaafu Mathew Mwaimu  amesema kwa kipindi cha hivi karibuni tume ya haki za Binadamu na utawala bora imeona katika vyombo vya habari zikihusisha ajali ya Naibu Waziri wa OR-TAMISEMI, Dkt Festo dugange na kifo cha Nusura Abdallah .



Jaji Mstaafu Mwaimu amesema taarifa hizo za vyombo vya habari zimeonekana kukinzana kutokana na taarifa zilizotolewa na jeshi la Polisi,Chuo kikuu cha Dodoma , Hospitali ya Faraja iliyopo Himo Mkoani Kilimanjaro na taarifa za wananchi kupitia mitandao ya kijamii.


Aidha Jaji Mstaafu Mwaimu amesema Tume inapoona kumetokea mashaka kutoka kwa wananchi kuhusu jambo lolote linaloashiria uvunjwaji wa haki za binadamu au mashaka ya haki kutokutendeka ina mamlaka ya kufanya uchuguzi juu ya jambo hilo.


Tarehe 3/5/2023 uongozi wa chuo kikuu cha UDOM ulipokea taarifa kutoka kwa mwanafunzi ambaye alikuwa anasoma naye kuwa amepokea taarifa kutoka kwa mtu aliyejitambulisha kuwa ni mjomba wa marehemu kuwa amefariki akiwa anapatiwa matibabu katika hospitali ya Faraja iliyopo Himo Kilimanjaro.


Marehemu Nusura alikuwa akisomea shahada ya kwanza ya Sanaa katika Elimu, katika Ndaki ya Insia na Sayansi ya Jamii.

Chapisha Maoni

0 Maoni