HakiElimu yabaini changamoto ya elimu dhidi ya jitihada za serikali


 Mkurugenzi wa HakiElimu Dk John Kalage amesema shirika hilo limebaini changamoto mbalimbali katika sekta ya elimu  licha ya  jitihada za serikali kuboresha sekta hiyo.

Dk Kalage   amesema changamoto ya  mlundikano wa wanafunzi darasani ipo na takwimu za elimu Tanzania  zinaonesha uwiano wa darasa shule za msingi ni 1:74 badala  ya 1:45 huku yale madarasa ya awali ukiwa ni 1:75 badala ya 1:40 unaotakiwa.


Akizungumzia kwa kina kuhusu utafiti huo na kuoanisha na ripoti ya CAG iliyobaini halmashauri 45 zina upungufu wa madawati 158,066 matundu ya vyoo 56,530, vyumba vya walimu 35,664 na upungufu wa madarasa 27,316 suala ambalo lisipotafutiwa ufumbuzi litazorotesha utoaji wa elimu.


Ametaja  changamoto nyingine ni uhaba wa walimu 100, 958 kwa shule za msingi sawa na asilimia 37 huku shule za sekondari uhaba wa walimu 74,743 sawa na asilimia 47 huku Tamisemi ikipewa kibali cha kuajiri walimu 13,130 tofauti ya hitaji la waalimu 162,571.


Dk Kalage amesema changamoto kubwa katika azma na mipango hii ni kukosekana kwa bajeti toshelezi ya utoaji mafunzo stahiki kwa waalimu walioko kazini, mathalani mwaka wa fedha 2020/21 serikali iliwezesha mafunzo kwa walimu wa juu ya utoaji wa ushauri na unasihi kutoka shule 174 kati ya 3,863 za sekondari saw ana asilimia 4.5.


Kwa mujibu wa ripoti ya Benki ya Dunia juu ya viashiria vya utoaji huduma katika mnyororo wa matokeo ya elimu (WB SDI Report, 2016) Idadi kubwa ya walimu bado hawana stadi za kitaaluma na uelimishaji zinazohitajika ili kufundisha ipasavyo.

Chapisha Maoni

0 Maoni