Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi, amesema Mkutano wa Tatu wa Tume ya Pamoja ya Kudumu ya Ushirikiano kati ya Tanzania na Oman (Joint Permanent Commission for Cooperation, JPC) ni fursa muhimu ya kuharakisha utekelezaji wa makubaliano na kupanua zaidi biashara, uwekezaji na ushirikiano wa maendeleo kati ya nchi hizo mbili.
Rais Dkt. Mwinyi ameyasema hayo leo, tarehe 10 Novemba 2026, Ikulu Zanzibar, alipokutana na Waziri wa Mambo ya Oman, Mhe. Sayyid Badr bin Hamad bin Hamood Albusaidi, aliyeko nchini kwa ziara ya kikazi na kushiriki Mkutano wa Tatu wa JPC uliofanyika Zanzibar.
Mhe. Albusaidi amefika Ikulu Zanzibar akiwa ameambatana na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Dkt. Mahmoud Thabit Kombo, Mhe. Maulidah Bwanakheir Hassan, Balozi wa Tanzania nchini Oman. pamoja na viongozi mbalimbali wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.
Rais Dkt. Mwinyi amesema uhusiano wa kihistoria na kindugu kati ya Zanzibar na Oman unapaswa kuendelea kutafsiriwa katika fursa halisi za kiuchumi na kijamii, huku akisisitiza umuhimu wa kutekeleza kwa wakati makubaliano yanayofikiwa kupitia JPC.
Amesema bado kuna nafasi kubwa ya kuongeza biashara na uwekezaji, hususan katika Uchumi wa Buluu, utalii, uvuvi na ufugaji wa samaki, na amewakaribisha wawekezaji wa Oman kutumia fursa zilizopo Zanzibar pamoja na kuimarisha mahusiano ya moja kwa moja kati ya wafanyabiashara wa Tanzania na Oman.
Rais Dkt. Mwinyi pia ameishukuru Serikali ya Oman kwa mchango wake katika sekta ya elimu, maji na uhifadhi wa urithi wa kihistoria Zanzibar, ikiwemo kusaidia mafunzo na ufadhili wa masomo pamoja na ukarabati wa maeneo mbalimbali ya kihistoria.
Kwa upande wake, Mhe. Albusaidi amesema Oman itaendelea kuimarisha uhusiano wa muda mrefu uliopo na Tanzania, akieleza kuwa JPC inatoa nafasi ya kusukuma mbele utekelezaji wa masuala yaliyofikiwa katika ziara na mazungumzo ya viongozi wa nchi hizo mbili.
Amesema kuna nafasi kubwa ya kukuza biashara, uwekezaji, utalii na mahusiano kati ya sekta binafsi, huku akieleza matarajio ya kuona kiwango cha biashara kati ya Tanzania na Oman kikiongezeka kwa kiasi kikubwa katika miaka ijayo.
Mhe. Albusaidi ameambatana na ujumbe wa Serikali ya Oman, akiwemo Balozi wa Oman nchini Tanzania, Mhe. Saud bin Hilal bin Saud Al Shaidani, na Balozi Mdogo wa Oman Zanzibar, Mhe. Said Salim Hamed Al Sinawi, pamoja na viongozi wengine wa Serikali ya Oman.

0 Maoni