Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Deogratius Ndejembi, ameonesha kutoridhishwa na kasi ya ujenzi wa barabara ya Amani Makoro - Ruanda yenye urefu wa kilomita 35, wilayani Mbinga, mkoani Ruvuma, baada ya mradi huo wenye thamani ya shilingi bilioni 60.5 kuchelewa kwa miaka miwili na miezi 10.
Akikagua maendeleo ya ujenzi wa barabara hiyo katika eneo la Amani Makoro, wilayani Mbinga, Makamu wa Rais amebaini kuwa ni kilomita 10.5 pekee zilizojengwa kati ya kilomita 35 zilizopangwa, licha ya mkataba wa awali wa ujenzi kuwa wa miezi 18.
Kutokana na hali hiyo, Makamu wa Rais ameiagiza Wizara ya Ujenzi kuandaa mpango kazi na mkakati madhubuti wa kuhakikisha mradi huo unakamilika, huku akisisitiza umuhimu wa kubaini na kushughulikia sababu zinazokwamisha utekelezaji wake.
Ameelekeza kuwa iwapo ucheleweshaji unasababishwa na mkandarasi, hatua stahiki zichukuliwe kwa kuzingatia sheria na taratibu za manunuzi ya umma. Aidha, iwapo changamoto inatokana na upatikanaji wa fedha, Serikali itafute ufumbuzi wa kuhakikisha fedha zinazohitajika zinapatikana ili kukamilisha mradi huo.
Akizungumza na wananchi wa Amani - Makoro, wakati wa ziara hiyo, Makamu wa Rais amesema Serikali ya Awamu ya Sita, chini ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, itaendelea kusimamia kwa karibu utekelezaji wa mradi huo ili kuhakikisha unakamilika na kuanza kutoa manufaa yaliyokusudiwa kwa wananchi.
Amesema kukamilika kwa barabara hiyo kutakuwa kichocheo muhimu cha maendeleo ya kiuchumi na kijamii kwa wananchi wa Wilaya ya Mbinga na Mkoa wa Ruvuma kwa ujumla, hususan katika kurahisisha shughuli za uzalishaji, biashara na usafirishaji.
Ameongeza kuwa barabara hiyo ina umuhimu wa kimkakati katika kuimarisha miundombinu inayohudumia shughuli za uwekezaji, ikiwemo miradi ya uchimbaji wa makaa ya mawe inayotekelezwa wilayani Mbinga.
Katika hatua nyingine, Makamu wa Rais amesisitiza kuwa dhamira ya Serikali ni kutatua changamoto zinazowakabili wananchi kwa kuhakikisha miradi ya maendeleo inatekelezwa kwa ufanisi na fedha za umma zinatumika kwa malengo yaliyokusudiwa.
Amesema Serikali itaendelea kuweka mbele maslahi ya wananchi, huku ikiimarisha usimamizi na uwajibikaji katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo ili kuzuia upotevu wa fedha na kuhakikisha thamani ya fedha inaonekana katika miradi inayotekelezwa.
Akizungumzia changamoto ya bei ya mahindi, Makamu wa Rais amewahakikishia wananchi kuwa Serikali inaendelea kushughulikia suala hilo ili kulinda maslahi ya wakulima na kuimarisha sekta ya kilimo.
Amewataka wananchi kuendelea kujikita katika uzalishaji wa mazao, hususan mahindi, na kuongeza kiwango cha uzalishaji katika msimu ujao wa kilimo.
Amesema Serikali inaendelea kufuatilia mwenendo wa bei ya mahindi na kuchukua hatua za kuhakikisha changamoto na makosa yaliyojitokeza katika upangaji wa bei hayajirudii.
Kwa upande wake, Mbunge wa Jimbo la Mbinga Vijijini, Mhe. Judith Kapinga, ameishukuru Serikali ya Awamu ya Sita kwa uwekezaji mkubwa katika miradi ya maendeleo mkoani Ruvuma, hususan katika Jimbo la Mbinga Vijijini.
Amesema uwekezaji huo una mchango mkubwa katika kuboresha huduma za kijamii, kuimarisha miundombinu na kufungua fursa mpya za kiuchumi kwa wananchi.
Hata hivyo, amesisitiza umuhimu wa kuhakikisha miradi inayoendelea kutekelezwa inakamilika kwa wakati ili wananchi waanze kunufaika na uwekezaji huo.
Aidha, ameiomba Serikali kuharakisha utekelezaji wa miradi mingine muhimu katika jimbo hilo, ikiwemo miradi ya maji, ili kuongeza upatikanaji wa huduma muhimu na kuboresha maisha ya wananchi.
Kukamilika kwa barabara ya Amani Makoro - Ruanda kunatarajiwa kuimarisha shughuli za kiuchumi, kurahisisha usafirishaji wa watu na bidhaa pamoja na kuchochea uwekezaji katika Wilaya ya Mbinga na Mkoa wa Ruvuma kwa ujumla.

0 Maoni