Dkt. Mwigulu: Zingatieni masilahi ya wananchi maeneo yenye madini

WAZIRI Mkuu, Dkt. Mwigulu Nchemba, amewataka maafisa madini kusimamia utaratibu unaozingatia masilahi ya wananchi katika maeneo yanayogundulika madini, badala ya kuwaondoa ili kupisha watu wengine.

Amesema masilahi ya mwenye shamba, mwenye leseni na mwekezaji yanapaswa kuzingatiwa ili shughuli za madini zichangie kubadilisha maisha ya wananchi.

Dkt. Mwigulu ametoa maelekezo hayo leo (Jumanne, Novemba 10, 2026), katika mkutano wa hadhara uliofanyika kata ya Majengo, Manispaa ya Kahama, mkoani Shinyanga.

“Waondoke waende wapi?” amehoji akizungumzia wananchi wanaotakiwa kuondoka baada ya madini kugundulika katika maeneo hayo.

Amemtaka Naibu Waziri wa Madini, Dkt. Steven Kiruswa, kusimamia utaratibu uliowekwa ili wahusika wanufaike.

“Utaratibu huo, Mheshimiwa Naibu Waziri, usimamiwe. Ni mzuri mno, unabadilisha maisha ya Watanzania,” amesema.

Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu ameonya dhidi ya matumizi mabaya ya amri za mahakama katika ukusanyaji wa madeni, ikiwemo kuuza dhamana kwa bei ndogo kuliko thamani yake wakati sehemu kubwa ya deni imelipwa.

“Hatuwezi watu wakawa umeshalipa asilimia 80, umeshalipa asilimia 90, halafu dhamana yako yote inaenda inauzwa,” amesema.

Amesema iwapo kuna mianya ya kisheria inayotumiwa kuwaumiza wananchi, Serikali itatafuta ushauri ili maeneo hayo yaangaliwe upya.

Kauli hiyo imefuatia malalamiko ya mfanyabiashara wa Soko la Kahama Mjini, Salum Abdallah Amani, kuhusu kuchukuliwa kwa bidhaa zake. Viongozi waliojibu wameeleza kuwa hatua hiyo ilihusiana na utekelezaji wa amri ya mahakama kuhusu deni la shilingi milioni mbili.

Waziri Mkuu amemwelekeza Mkuu wa Kitengo cha Huduma za Sheria wa Manispaa ya Kahama, Steven Magalla, kupitia nyaraka na kuwasikiliza wahusika ili haki itendeke kwa pande zote.

Kuhusu ombi la kurejeshwa kwa adhabu ya viboko shuleni lililowasilishwa na mwananchi Jackson Mkama, Dkt. Mwigulu amesisitiza umuhimu wa wazazi na jamii kushiriki malezi ya watoto, badala ya kuwaachia walimu na wafanyakazi wa nyumbani jukumu hilo.

Amesema utamaduni wa mtoto kuonywa na mtu mzima yeyote alipokosea umedhoofika, huku baadhi ya wazazi wakipinga watoto wao kuonywa na watu wengine.

“Lazima tuwekeze kwenye malezi ya watoto wetu,” amesema.

Kuhusu afya, Waziri Mkuu amemwelekeza Mkurugenzi wa Manispaa ya Kahama kukamilisha maandalizi ya kitaalamu na taratibu za manunuzi kwa ajili ya jengo la huduma za dharura katika Hospitali ya Manispaa hiyo, ili ujenzi uanze katika mwaka ujao wa fedha.

Awali, amekagua ujenzi wa jengo la mama na mtoto la shilingi bilioni 6.79, ambalo limefikia asilimia 70 ya utekelezaji, na kuipongeza manispaa kwa kutumia mapato ya ndani pamoja na mchango wa Serikali Kuu kutekeleza mradi huo.

Chapisha Maoni

0 Maoni