TFS yaipeleka Tanzania duniani kupitia IPU 153, yatangaza fursa za utalii wa misitu na malikale


Na. Mwandishi Wetu- Arusha 

ARUSHA: Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) unatumia jukwaa la kimataifa la Mkutano wa 153 wa Umoja wa Mabunge Duniani (IPU 153) kutangaza fursa za utalii wa misitu na malikale, uwekezaji na uhifadhi wa rasilimali zinazopatikana Tanzania.

TFS ni miongoni mwa taasisi zinazoiwakilisha Tanzania katika maonesho yanayoambatana na mkutano huo unaofanyika katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano Arusha (AICC), Oktoba 5–9, 2026, ukiwakutanisha wajumbe kutoka mabunge mbalimbali duniani.

Akizungumza katika maonesho hayo mapema hivi Leo, 5 Octoba 2026, Afisa Utalii wa TFS, Salome Kivuyo, alisema ushiriki wa TFS katika IPU 153 ni fursa muhimu ya kuitangaza Tanzania kimataifa kupitia utajiri wa misitu na malikale zinazopatikana katika maeneo mbalimbali nchini.

“Tunatumia jukwaa hili kuwaonesha wageni kutoka sehemu mbalimbali duniani fursa zilizopo katika utalii wa misitu na malikale, pamoja na umuhimu wa kuhifadhi rasilimali hizi kwa manufaa ya kizazi cha sasa na kijacho,” alisema Kivuyo.

Kupitia banda la Wizara ya Maliasili na Utalii, TFS inawafikia wajumbe na wageni wa kimataifa kwa kuwaonesha vivutio vya utalii vinavyopatikana katika misitu, pamoja na maeneo yenye thamani ya malikale, huku ikieleza fursa za uwekezaji na ushirikiano katika sekta hiyo.

Kivuyo aliwaalika wajumbe wa IPU 153, washiriki wa mkutano na wageni kutoka ndani na nje ya Tanzania kutembelea banda la TFS ili kupata fursa ya kujifunza zaidi kuhusu utajiri wa misitu na malikale za Tanzania, vivutio vya utalii pamoja na fursa za uwekezaji.

Ushiriki huo unaifanya Tanzania kutumia jukwaa la IPU 153 kuongeza uelewa wa kimataifa kuhusu utajiri wa rasilimali za misitu na malikale nchini, huku ukifungua milango ya ushirikiano na uwekezaji katika utalii unaozingatia uhifadhi na matumizi endelevu ya rasilimali.



Chapisha Maoni

0 Maoni