Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii anayeshughulikia Masuala ya Utalii, Nkoba Mabula, amesema matumizi ya teknolojia na akili unde (AI) ni fursa muhimu katika kukuza sekta ya utalii nchini.
Mabula amesema Tanzania inapaswa kuhakikisha vivutio vyake vinaonekana katika majukwaa ya kidijitali yanayotumiwa na watalii kutafuta taarifa kuhusu nchi, vivutio, maeneo ya malazi na kupanga ratiba za safari.
Amesema hayo akiwa Mgeni Rasmi katika Mkutano wa Nne wa Kimataifa wa Utalii 2026 jijini Arusha, wenye kaulimbiu "Ajenda ya Kidijitali na Akili Unde ili Kuunda Upya Utalii".
Kwa upande wake, Profesa Eliamani Sedoyeka kutoka Chuo cha Uhasibu Arusha (IAA), amesema AI inabadilisha namna watalii wanavyopanga safari, ikiwemo kuchagua nchi, vivutio, malazi na usafiri.
Amesema mabadiliko hayo yanatoa fursa kwa Tanzania kuongeza mguso wa kibinadamu katika huduma za utalii, huku taasisi za elimu zikiendelea kufanya tafiti, kutoa ushauri wa kitaalamu na kuandaa wataalamu watakaokidhi mahitaji mapya ya sekta ya utalii katika zama za teknolojia na AI.

0 Maoni