Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Mhe. Prof. Riziki Shemdoe (Mb) ameridhishwa na maendeleo ya utekelezaji wa mradi wa ujenzi wa barabara zinazoingia katika uwanja wa AFCON mkoani Arusha ambapo utekelezaji wake umefikia asilimia 71.
Akiwa katika ziara ya kukagua maendeleo ya mradi huo, Prof. Shemdoe ameipongeza Wakala ya Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) kwa usimamizi na utekelezaji wa mradi huo huku akimtaka Mkandarasi kuongeza kasi ya kazi na kuhakikisha anakamilisha ujenzi kwa wakati kwa kuzingatia viwango vya ubora vilivyowekwa kwenye mkataba.
"Mradi huu unatekelezwa vizuri na hatua iliyofikiwa inaonesha kuwa kazi inaendelea kwa kasi inayotarajiwa, hivyo ni muhimu mkandarasi kuhakikisha anakamilisha mradi huu kwa wakati kama ilivyoainishwa katika mkataba ili miundombinu hii iwe tayari kwa matumizi yaliyokusudiwa," amesema Prof. Shemdoe.
Aidha, Prof. Shemdoe amempongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuwezesha upatikanaji wa fedha za utekelezaji wa mradi huo unaohusisha ujenzi wa jumla ya kilomita 19.9 za barabara kwa kiwango cha lami.
Amesisitiza kuwa ujenzi wa barabara hizo ni sehemu muhimu ya maandalizi ya Tanzania kuwa mwenyeji wa michuano ya Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) mwaka 2027 kwani utaimarisha huduma za usafiri na usafirishaji na kurahisisha wachezaji, viongozi, wageni na mashabiki watakaohudhuria michuano hiyo kufika uwanjani kwa urahisi.
Ameongeza kuwa maandalizi ya michuano hiyo yanahitaji miundombinu imara na yenye ubora hususan barabara zitakazounganisha maeneo mbalimbali na uwanja wa michezo ili kuhakikisha washiriki na wageni wanapata huduma bora wakati wote wa mashindano.
Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Arusha Mhe. Nicodemus Tambo amesema ataendelea kufuatilia na kusimamia kwa karibu utekelezaji wa mradi huo ili kuhakikisha unakamilika kwa wakati, unakidhi viwango vilivyowekwa na kuanza kutoa huduma kwa wananchi pamoja na wageni watakaotembelea mkoa huo wakati wa michuano ya AFCON 2027.


0 Maoni