Uwezeshaji vijana kiuchumi wachochea viwanda vipya

Mwamko wa vijana nchini kuanzisha viwanda vidogo umeendelea kuongezeka kwa kasi kutokana na jitihada za serikali za kuwawezesha kiuchumi kupitia miradi na programu mbalimbali, ambapo Kaimu Meneja wa Shirika la Kuhudumia Viwanda Vidogo (SIDO) Mkoa wa Dodoma, Nyangusi Meitelani ameeleza kuwa vijana wengi wameanza kutambua fursa zilizopo katika sekta ya uzalishaji na kugeukia uanzishaji wa viwanda hivyo.

Akizungumza na moja ya magazeti nchini, Meitelani alisema SIDO imekuwa ikitoa elimu, mafunzo na ushauri kwa vijana kuhusu ubunifu wa bidhaa, matumizi ya teknolojia, ufungashaji, utafutaji wa masoko, pamoja na teknolojia za uongezaji thamani wa mazao ya kilimo na mifugo, usindikaji wa vyakula na utengenezaji wa bidhaa za ngozi.

Alibainisha kuwa kwa Mkoa wa Dodoma kuna teknolojia rafiki zenye gharama kuanzia Sh milioni 1.5 na kuendelea kwa ajili ya kuongeza thamani ya karanga na kusindika nafaka kama mahindi na mtama.

Meitelani aliongeza kuwa vijana wameamka na wanatafuta fursa katika mnyororo mzima wa uzalishaji, huku baadhi wakiungana kufanya miradi ya pamoja, jambo ambalo ni muhimu katika kujenga uchumi wa mtu mmoja mmoja na taifa kwa ujumla.

Aliwahimiza vijana kutumia rasilimali na malighafi zinazopatikana katika maeneo yao badala ya kuuza bidhaa ghafi ili kuongeza kipato na ajira, huku akiwataka kutafuta taarifa sahihi na kutumia wataalamu na taasisi za uwezeshaji ili kuhakikisha biashara zao zinakuwa endelevu, zinazoongeza bidhaa zinazotengenezwa nchini, na kupunguza utegemezi wa bidhaa kutoka nje.

 

Chapisha Maoni

0 Maoni