Uchumi kidijiti washika kasi: Laini milioni 62 za intaneti zazaa fursa mpya za ajira na biashara

Serikali imetangaza kuwa uchumi wa kidijiti unazidi kuimarika nchini, huku Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Angellah Kairuki akieleza kuwa sekta ya mawasiliano imeendelea kukua na kuwa sehemu muhimu ya maendeleo ya kiuchumi na kijamii kupitia ongezeko la matumizi ya simu, intaneti, utangazaji, posta na usafirishaji wa vifurushi.

Akitoa Taarifa ya Hali ya Sekta ya Mawasiliano kwa robo mwaka katika ofisi za Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) jijini Dar es Salaam, Waziri Angellah alibainisha kuwa laini za simu zimeenea kwa asilimia 167 na simu hizo zimekuwa miundombinu inayowezesha biashara, elimu, ajira, huduma za fedha na mawasiliano ya kila siku kwa wananchi.

Ukuaji huo unatoa fursa kubwa kwa vijana wanaokesha mitandaoni kujifunza na kutumia fursa za kiuchumi, hasa ukizingatia kuwa matumizi ya intaneti na data yamekua kwa kasi na laini zilizotumika kupata huduma za intaneti ziliongezeka kutoka 58,814,327 mwezi Machi 2026 hadi kufikia 62,595,289 mwezi Juni 2026.

Kupitia miundombinu hiyo na upanuzi wa minara mipya 758 iliyozinduliwa Aprili 10, mwaka huu—iliyoongeza upatikanaji wa mawasiliano kwa watu milioni 8.5 katika vijiji 1,400 nchini—vijana wanapaswa kuachana na matumizi yasiyo na tija na badala yake kugeuza mitandao kuwa rasilimali ya kibiashara, huku wakijifunza umuhimu wa uaminifu mtandaoni kutokana na ukweli kwamba matukio ya ulaghai na utapeli kupitia simu za mkononi yamepungua kwa asilimia 25.29 kutoka matukio 9,816 ya robo iliyoishia Machi 2026 hadi kufikia matukio 7,334 mwezi Juni mwaka huo baada ya TCRA kuchukua hatua dhidi ya laini zilizohusika na vitendo hivyo.

Aidha, mfumo jumuishi wa kifedha umezidi kuimarika na unatoa mtaji wa kimawasiliano kwa vijana wanaotaka kujiajiri, ambapo asilimia 74.5 ya laini za simu zinazotumika zina akaunti za huduma za fedha za mtandao, huku akaunti hizo zikiongezeka kwa asilimia 7.5 kutoka akaunti 80,977,268 hadi kufikia 87,046,089 kati ya Machi na Juni 2026.

Ongezeko hili linawawezesha vijana kufanya biashara mtandaoni, kupokea malipo, na kusimamia miamala yao ya kifedha kwa usalama na urahisi bila kubeba fedha taslimu, jambo ambalo linapaswa kuwahamasisha kujikita katika ujasiriamali wa kidijiti ili kujiletea maendeleo binafsi na kuchangia uchumi wa taifa.

Chapisha Maoni

0 Maoni