Rais Samia aagana rasmi na Balozi wa Misri nchini

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, amekutana na Balozi wa Jamhuri ya Kiarabu ya Misri nchini, Sherif Ismail, aliyefika Ikulu jijini Dar es Salaam kumuaga rasmi baada ya kumaliza muda wake wa utumishi nchini.

Katika mazungumzo hayo, Rais Samia amemshukuru Balozi Ismail kwa mchango wake katika kuimarisha uhusiano wa muda mrefu na wa kirafiki kati ya Tanzania na Misri katika kipindi cha miaka minne ya utumishi wake nchini.

Rais Samia amesema Tanzania na Misri zimeendelea kuimarisha ushirikiano katika sekta mbalimbali, ikiwemo biashara na uwekezaji, elimu, afya, kilimo, nishati, utalii, usafiri na uchukuzi.

Aidha, amesisitiza umuhimu wa kuendelea kupanua biashara na uwekezaji kati ya nchi hizo ili kutumia kikamilifu fursa zilizopo na kuwaletea manufaa wananchi wa pande zote mbili.

Mazungumzo hayo pia yamegusia umuhimu wa kuboresha miundombinu na huduma za usafiri na uchukuzi ili kurahisisha biashara kati ya Tanzania na Misri, pamoja na masoko mengine barani Afrika.

Katika sekta ya elimu, Rais Samia ameishukuru Misri kwa kuendelea kutoa ufadhili wa nafasi za masomo, mafunzo na programu mbalimbali za kuwajengea uwezo Watanzania.

Viongozi hao pia wamejadili namna ya kuimarisha ushirikiano katika sekta ya afya, ikiwemo kutoa mafunzo kwa wataalamu, kuboresha upatikanaji wa vifaa tiba na kuendeleza uzalishaji wa dawa.

Kwa upande wake, Balozi Ismail amemshukuru Rais Samia, Serikali na wananchi wa Tanzania kwa ushirikiano, msaada na ukarimu alioupata katika kipindi chote cha utumishi wake nchini.

Amesema miaka yake minne nchini Tanzania imekuwa sehemu muhimu na ya kukumbukwa katika utumishi wake, huku akisisitiza kuwa urafiki kati ya Tanzania na Misri utaendelea kudumu.

Rais Samia amemtakia Balozi Ismail mafanikio katika majukumu yake yajayo na kueleza imani kuwa uhusiano kati ya Tanzania na Misri utaendelea kuimarika kwa manufaa ya wananchi wa nchi zote mbili.

Bakari S. Machumu

Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, Ikulu

Chapisha Maoni

0 Maoni