Dkt. Akwilapo atolea ufafanuzi malalamiko ya wananchi kuhusu migogoro ya ardhi

Na. Munir Shemweta, Dodoma

Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Mhe. Dkt. Leonard Akwilapo, ametolea ufafanuzi malalamiko yanayohusu migogoro ya ardhi katika maeneo mbalimbali nchini, huku akisisitiza wananchi kuzingatia sheria na taratibu za umiliki na matumizi ya ardhi ili kuepuka migogoro na hasara zinazoweza kujitokeza.

Mhe. Dkt. Akwilapo amesema hayo Agosti 26, 2026, ofisini kwake Mtumba jijini Dodoma, alipokutana na waandishi wa habari kutoa ufafanuzi kufuatia malalamiko ya baadhi ya wananchi kuhusu kuvunjiwa maendelezo waliyoyafanya kwenye maeneo mbalimbali nchini. Aidha, kumekuwa na malalamiko mengine yanayohusu matumizi na umiliki wa baadhi ya maeneo ya ardhi.

Kwa mujibu wa Dkt. Akwilapo, ufuatiliaji wa karibu uliofanywa na Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi umebaini kuwa baadhi ya wananchi wanaowasilisha malalamiko hayo hawatoi taarifa sahihi kuhusu uhalisia wa masuala yao, huku wengine wakitumia mitandao ya kijamii na vyombo vya habari kutafuta huruma ya jamii. Amesisitiza kuwa Serikali imekuwa ikifuatilia kwa kina kila suala linalowasilishwa ili kuhakikisha ukweli unabainika na haki inatendeka kwa mujibu wa sheria.

Akitoa mifano ya baadhi ya matukio hayo, Mhe. Dkt. Akwilapo ametaja tukio la Agosti 18, 2026, linalomhusisha Bi. Rahel Suda dhidi ya Bi. Adelaida Mkoko kuhusu umiliki wa Kiwanja Na. 42, Kitalu B, kilichopo Kikuyu Extension jijini Dodoma, ambapo Wizara tayari imeshatoa ufafanuzi kuhusu suala hilo baada ya kupata maelezo ya kina.

Tukio lingine ni la Agosti 22, 2026, linalomhusisha Bw. Maulid Juma dhidi ya Mhe. Diwani wa Kata ya Makulu, Dodoma, kuhusu Kiwanja Na. 212, Medeli, ambacho kwa mujibu wa nyaraka zilizopo kinamilikiwa na Adam Saimon Slay, aliyepewa nyaraka za umiliki tangu kipindi cha Mamlaka ya Ustawishaji Makao Makuu (CDA). Aidha, Waziri ametaja matukio mengine nane yaliyoripotiwa katika vipindi tofauti kati ya Januari na Agosti 2026.

Malalamiko mengine kwa mujibu wa Mhe. Dkt Akwilapo yanahusisha utekelezaji wa hatua zinazochukuliwa na mamlaka zenye wajibu wa kisheria wa kusimamia maeneo ya hifadhi za miundombinu, ikiwemo umeme na reli. "Maeneo mengine yenye malalamiko ni yale yanayohusu utekelezaji wa hatua za mamlaka zenye wajibu wa kisheria wa kusimamia hifadhi za umeme au reli katika maeneo ya Tegeta kwa Ndevu, Mavurunza na Kilungule, mkoani Dar es Salaam," amesema Mhe. Dkt. Akwilapo.

Ameongeza kuwa Wizara inatambua umuhimu wa mitandao ya kijamii katika kufikisha taarifa na malalamiko ya wananchi serikalini, lakini akabainisha kuwa baadhi ya watu wamekuwa wakiitumia kutoa taarifa zisizo sahihi, licha ya kufahamu kuwa masuala yao tayari yameshughulikiwa kwa kuzingatia maamuzi ya mahakama au hatua za kisheria zilizochukuliwa na Serikali. Amesema hatua hizo hulenga kulinda haki za ardhi za wananchi wengine, pamoja na kuhakikisha mipango ya uendelezaji wa miji iliyoidhinishwa inatekelezwa kwa mujibu wa sheria.

"Napenda kutoa rai kwa wananchi kuzingatia taratibu za kisheria katika kupata ardhi na kufanya ujenzi mijini na vijijini ili kuepuka kupata hasara kutokana na kubomolewa kwa maendelezo yaliyofanyika kinyume cha sheria," amesema Dkt. Akwilapo.

Aidha, amewahimiza wananchi wenye changamoto za ardhi kufuata taratibu rasmi za kuwasilisha malalamiko yao katika ofisi husika za Serikali ili yaweze kufanyiwa kazi ipasavyo, kwa wakati na kwa kuzingatia sheria.

Chapisha Maoni

0 Maoni