Wananchi
wanaotembelea banda la Tume ya Madini katika Maonesho ya 50 ya Biashara ya
Kimataifa ya Dar es Salaam (SabaSaba) wanaendelea kunufaika na elimu kuhusu
matumizi ya kifaa cha Gemmological Torch, kinachotumika kutambua ubora na
thamani halisi ya madini ya vito.
Akitoa elimu
katika banda hilo, Mjiolojia na Mjimolojia Mwandamizi kutoka Ofisi ya Afisa
Madini Mkazi Mirerani, Selemani Khamisi, amesema thamani ya madini ya vito
hupimwa kwa kuzingatia vigezo vinne vikuu vinavyojulikana kitaalam kama 4Cs, ambavyo
ni rangi (Colour), uzito (Carat), ubora (Clarity) na umbo la ukataji (Cut).
Amesema
pamoja na matumizi ya Gemmological Torch, wataalam pia hutumia vifaa vingine
vya kitaalam ikiwemo Head Loupe, Table Lamp na Price Guide ya Serikali ili
kufanya tathmini ya kina ya ubora wa jiwe.
Uchunguzi
huo huwezesha kubaini nyufa, mipasuko, uchafu wa ndani (inclusions), pamoja na
ubora na ukolezi wa rangi ya jiwe.
“Kadiri jiwe
linavyokuwa na rangi ang’avu, ubora mzuri wa ndani, uzito mkubwa na ukataji
mzuri, ndivyo thamani yake inavyoongezeka. Matumizi ya vifaa kama Gemmological
Torch na Head Loupe hutuwezesha kubaini sifa hizo kwa usahihi,” amesema
Khamisi.
Ameongeza
kuwa madini ya vito yaliyovutia zaidi wananchi wanaotembelea banda la Tume ya
Madini ni Tanzanite ghafi na iliyoongezwa thamani, Green Garnet, Tourmaline na
Almandite Garnet, ambapo wageni wamekuwa wakipata fursa ya kujifunza sifa,
ubora na thamani ya kila aina ya jiwe la vito.
Khamisi
amewahimiza wananchi, wafanyabiashara wa madini na wadau wengine wa sekta ya
madini kutembelea banda la Tume ya Madini ili kujifunza matumizi ya vifaa vya
kisasa vya uchunguzi wa madini ya vito, vinavyosaidia kufanya tathmini sahihi
ya ubora na thamani ya madini hayo kabla ya kuyauza au kuyanunua.
Amesema
elimu hiyo ni sehemu ya juhudi za Tume ya Madini za kuongeza uelewa wa umma
kuhusu biashara ya madini ya vito, kuimarisha uwazi katika biashara hiyo na
kuongeza thamani ya rasilimali za madini nchini.

.jpeg)

0 Maoni