Shirika la
Fedha la Kimataifa (IMF) limeidhinisha kutolewa mara moja kwa takriban dola za
Marekani milioni 443.9, ambazo ni sawa na zaidi ya shilingi trilioni 1.2 za
Kitanzania, baada ya kukamilisha tathmini za mwisho chini ya programu mbili za
kimkakati.
Fedha hizo
zinalenga kuimarisha uchumi wa nchi kupitia sekta za uzalishaji na huduma za
jamii chini ya mpango wa Extended Credit Facility (ECF) uliotengewa dola
milioni 158.75, pamoja na kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi
chini ya mpango wa Resilience and Sustainability Facility (RSF) uliopata dola
milioni 298.37.
Uamuzi huo
uliotangazwa kwenye taarifa rasmi ya shirika hilo kufuatia kukamilika kwa
mapitio ya sita na saba ya ECF pamoja na mapitio ya tatu na nne ya RSF,
unaashiria kuendelea kwa imani kubwa ya taasisi hiyo kwa mwenendo na usimamizi
wa kiuchumi wa nchi.
Ripoti ya
IMF imeonyesha kuwa uchumi wa Tanzania umeendelea kuonyesha uimara mkubwa, huku
ukuaji wa Pato la Taifa ukifikia asilimia 5.9 mwaka 2025 na kutarajiwa kushika
kasi hadi kufikia karibu asilimia 6.2 kwa muda wa kati.
Ukuaji huu
unachochewa kwa kiasi kikubwa na ufanisi katika sekta za madini, kilimo, na
utalii, sambamba na udumishaji wa utulivu wa uchumi mpana uliowezesha mfumuko
wa bei kubaki chini ya asilimia 4.0.
Naibu
Mkurugenzi Mtendaji wa IMF na Kaimu Mwenyekiti wa Bodi, Bw. Bo Li, ameisifu
Tanzania kwa kulinda utulivu huo licha ya misukosuko ya ndani na nje, ingawa
alibainisha kuwa kupanda kwa bei za mafuta duniani na kuendelea kwa mzozo wa
Mashariki ya Kati kunaweza kuleta shinikizo kwenye gharama za maisha na ukuaji
wa uchumi.
Katika
utekelezaji wa mageuzi ya kiuchumi, IMF imeridhishwa na jinsi vigezo vingi vya
utendaji vilivyofikiwa kwa wakati, ingawa ilibainisha kuchelewa kwa baadhi ya
malengo katika maeneo ya nishati, usimamizi wa kodi ya VAT, utawala wa Benki
Kuu, na uwekezaji wa umma. Shirika hilo limeishauri serikali kuongeza kasi
katika kuimarisha ukusanyaji wa mapato ya ndani, kuboresha usimamizi wa fedha
za umma, na kuongeza uwekezaji kwenye huduma za kijamii kama elimu na afya ili
kukabiliana na changamoto za muda mrefu za kupunguza umaskini na kuandaa fursa
kwa idadi ya watu inayokua.
Akipokea
maamuzi hayo, Waziri wa Fedha, Mhe. Balozi Khamis Mussa Omar, ametoa shukrani
zake za dhati kwa IMF kwa kuendelea kuamini na kuunga mkono mageuzi makubwa ya
kiuchumi na kijamii ambayo nchi inapiga hatua hadi sasa. Ushirikiano huu wa
kihistoria kati ya Tanzania na IMF ulioanza tangu tarehe 10 Septemba 1962,
umeshuhudia jumla ya ahadi za mikopo na misaada zikifikia dola bilioni 4.578,
huku kiasi cha sasa kinachoendelea kufanya kazi kikiwa ni dola bilioni 2.52
ambazo zinaendelea kuleta msukumo mpya katika ustahimilivu na maendeleo
endelevu ya taifa.

0 Maoni