Wafanyakazi wa Nyumbani Wahimizwa Kutumia Mifumo ya Kidijitali Kudai Haki

  

Wafanyakazi wa nyumbani wametakiwa kutumia mifumo ya kidijitali ili kufuatilia na kudai haki zao pindi wanapokumbana na changamoto za ukandamizaji au migogoro mahali pa kazi. 

Wito huo umetolewa na Mkurugenzi wa Tume ya Usuluhishi na Uamuzi (CMA), Usekelege Mpulla, wakati akifungua mafunzo maalum mkoani Morogoro yaliyoandaliwa na Shirika la Kazi Duniani (ILO) kwa kushirikiana na Chama cha Kutetea Watumishi wa Hifadhi, Majumbani, Watoa Huduma na wa kwenye Mahoteli (CHODAWU). 

Akizungumza katika mafunzo hayo, Mpulla amewahimiza wafanyakazi hao kutokujiona wanyonge kwa kusisitiza kuwa sheria za Tanzania zinawatambua na kuwalinda kikamilifu, hivyo hawapaswi kukubali kunyimwa haki zao za msingi. 

Aidha, amebainisha kuwa Tume ya Usuluhishi na Uamuzi (CMA) iko tayari kupokea na kushughulikia migogoro ya wafanyakazi wote bila ubaguzi, huku kipaumbele kikielekezwa kwa wafanyakazi wa nyumbani kutokana na mazingira magumu wanayofanyia kazi. 

Waziri amesisitiza kuwa Tanzania inaendelea kuimarisha mifumo yake ya kulinda haki za wafanyakazi kwa kufuata viwango vya kimataifa, lengo likiwa ni kuhakikisha kila mfanyakazi anapata haki yake kwa usawa na kwa mujibu wa sheria.

Chapisha Maoni

0 Maoni