Rais Samia awataka viongozi kutafsiri vipaumbele vya serikali

 

Na. Bakari S. Machumu -Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, Ikulu

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, amewataka viongozi wa Serikali kufanya kazi kwa bidii, kusimamia vipaumbele vya Serikali na kuhakikisha dhamana wanazopewa zinaleta matokeo yanayoonekana kwa wananchi.

Rais Dkt. Samia ameyasema hayo leo Ikulu, Dar es Salaam, baada ya kuwaapisha viongozi wapya aliowateua hivi karibuni katika nafasi mbalimbali za utumishi wa umma.

Dhamana mlizopewa ni zaidi ya vyeo. Nendeni mkazitendee haki kwa kufanya kazi kwa bidii na uadilifu, mkiwatumikia wananchi,” amesema Rais Dkt. Samia.

Amewataka viongozi hao kusukuma vipaumbele vya Serikali kwa kasi na matokeo, akisema wanaanza kazi wakati Serikali ikianza utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo

2050 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa mwaka 2026/2027.

Katika sekta ya afya, Rais Dkt. Samia amesisitiza usimamizi makini wa bajeti, vipaumbele na rasilimali zilizopo ili huduma ziwafikie wananchi kwa haraka na kwa ubora unaotakiwa.

Amesema Serikali inalenga kuongeza uzalishaji wa dawa, vifaa tiba na chanjo nchini ili kupunguza utegemezi wa bidhaa hizo kutoka nje, kuongeza upatikanaji wa huduma za afya nchini, na kubana matumizi ya fedha za nchi katika uagizaji wa bidhaa hizo.

Lengo letu ni kufikia angalau asilimia 60 ya uzalishaji wa ndani wa dawa, vifaa tiba na chanjo ifikapo mwaka 2030. Wakaribisheni wawekezaji kwenye eneo hili, lakini kwa kuzingatia ubora,” amesema Rais Dkt. Samia.

Akizungumzia Jumuiya ya Afrika Mashariki, Rais Dkt. Samia ameitaka Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki kuendelea kusimamia maslahi ya Tanzania katika biashara, uchumi na fursa za maendeleo, na kuimarisha Jumuiya hiyo.

Aidha, Rais Dkt. Samia ameitaka Tume ya Utumishi wa Umma kusimamia mashauri, malalamiko na migogoro ya watumishi kwa uwazi na haki, ili kuendelea kujenga nidhamu, uadilifu na imani katika utumishi wa umma.

Viongozi walioapishwa ni Dkt. Grace Elias Magembe kuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya; Bw. Charles Ngeleja Kadonya kuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, anayeshughulikia masuala ya Afrika Mashariki; na Bw. Nolasco Jacob Kipanda kuwa Katibu wa Tume ya Utumishi wa Umma.





Chapisha Maoni

0 Maoni