Prof. Malami aisifu ORCI kwa mageuzi makubwa ya huduma za Saratani

  

Mtaalamu wa masuala ya usajili wa visa vya saratani na kanzi data kutoka African Cancer Registry Network (AFCRN) Prof. Sani Malami amesema maboresho makubwa yaliyofanywa na Taasisi ya Saratani Ocean Road (ORCI) katika huduma za uchunguzi na matibabu ya saratani yameongeza uwezo wa Tanzania kutoa huduma za kibingwa ndani na nje ya nchi hatua inayowawezesha wagonjwa wengi kupata matibabu kwa wakati bila kulazimika kusafiri nje ya nchi. 

Prof. Sani Malami ambaye pia ni Mkuu wa Kitengo cha Ufuatiliaji wa Saratani katika Taasisi ya Tiba na Utafiti wa Saratani ya Nigeria alitoa kauli hiyo leo alipotembelea ORCI kwa lengo la kujifunza mfumo wa usajili wa saratani (Cancer Registry) unaotekelezwa na taasisi hiyo ili uzoefu huo uweze kutumika kuimarisha huduma kama hizo nchini Nigeria. 

Alisema alitembelea ORCI kwa mara ya kwanza miaka 10 iliyopita na mwaka jana, lakini katika ziara yake ya sasa ameshuhudia taasisi hiyo ikiwa imepiga hatua kubwa katika miundombinu, matumizi ya teknolojia za kisasa na utoaji wa huduma bora kwa wagonjwa. 

"Nimeona mabadiliko makubwa tangu nilipofika hapa mara ya kwanza. Uwekezaji uliofanyika ni mkubwa na unaonyesha dhamira ya dhati ya kuboresha huduma za afya, hizi ni huduma zinazowanufaisha wagonjwa na zimeongeza ubora wa matibabu yanayotolewa katika taasisi hii",  alisema Prof. Malami. 

Aliongeza kuwa maboresho hayo yanaonekana kupitia ujenzi wa majengo ya kisasa, kuongezeka kwa wataalamu wa afya wenye ubingwa na ubobezi, upatikanaji wa vifaa tiba vya kisasa vya uchunguzi na matibabu pamoja na kuboreka kwa huduma zinazotolewa kwa wagonjwa wa saratani. 

"Ninawapongeza watumishi wa ORCI kwa kufanya kazi kwa weledi, kujituma na kuhakikisha wagonjwa wanapata huduma bora na kwa wakati kwa kutumia teknolojia za kisasa", alisema Prof. Malami. 

Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Saratani Ocean Road (ORCI) Dkt. Diwani Msemo alisema ujumbe huo kutoka Nigeria umefika nchini kufanya tathmini na kujifunza mfumo wa usajili wa saratani unaotekelezwa kupitia Kituo cha Usajili wa Saratani cha Mkoa wa Dar es Salaam kilichopo ORCI pamoja na vituo vingine vilivyopo nchini. 

Dkt. Msemo alisema Prof. Malami si mgeni katika taasisi hiyo kwani amewahi kutembelea ORCI mara mbili jambo lililomwezesha kushuhudia kwa karibu maendeleo makubwa yaliyopatikana katika utoaji wa huduma kwa kipindi hicho. 

Alieleza kuwa wageni hao walitembelea idara mbalimbali za ORCI na kujionea maboresho yaliyofanyika katika miundombinu, vifaa tiba, huduma za kitabibu pamoja na mfumo wa usajili wa saratani. 

Dkt. Msemo alisema mafanikio hayo yametokana na uwekezaji mkubwa unaoendelea kufanywa na Serikali katika sekta ya afya. 

"Ninaishukuru Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa uwekezaji mkubwa uliofanyika katika sekta ya afya. Ujenzi wa majengo ya kisasa, ununuzi wa vifaa tiba vya kisasa na uwekezaji katika kuwajengea uwezo wataalamu wa afya kupitia mafunzo ya ubingwa na ubobezi umeongeza kwa kiasi kikubwa ubora wa huduma za afya na kuwezesha wananchi kupata huduma za kibingwa hapa nchini",  alisema Dkt. Msemo. 

Ziara ya ujumbe huo kutoka Nigeria inaonyesha jinsi uwekezaji unaoendelea katika sekta ya afya ulivyochangia kuimarika kwa huduma za saratani nchini na kuifanya ORCI kuwa miongoni mwa taasisi zinazovutia wataalamu kutoka mataifa mbalimbali barani Afrika kwenda kujifunza na kubadilishana uzoefu. 

Prof. Malami ametembelea Tanzania kupitia African Cancer Registry Network (AFCRN) kwa madhumuni ya kubadilishana uzoefu na kujifunza mbinu bora zinazotumika katika uratibu wa usajili wa visa vya saratani, mifumo ya ufuatiliaji wa wagonjwa wa saratani na usimamizi wa Kitengo cha Kitaifa cha Usajili wa visa vya Saratani kilicho chini ya Wizara ya Afya. 

African Cancer Registry Network (AFCRN) ni mtandao unaoratibu na kuimarisha shughuli za usajili wa saratani barani Afrika  kwa lengo la kuboresha ubora wa takwimu za visa vya saratani, kuimarisha tafiti na kusaidia nchi wanachama kupanga na kutekeleza huduma za kinga, uchunguzi na matibabu ya saratani kwa ufanisi.

Chapisha Maoni

0 Maoni