Na. Mwandishi Wetu, Chalinze
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Mhandisi Hamad Yussuf Masauni, amesema Muungano wa Tanzania ni tunu ya taifa isiyopaswa kuchezewa na kwamba kila Mtanzania ana wajibu wa kuulinda kwa kuwa ndiyo alama kubwa ya umoja wa nchi.
Masauni amesema hayo Julai 22, 2026, wilayani Bagamoyo, mkoani Pwani, alipokuwa katika ziara ya kikazi, ambapo alieleza kufurahishwa na kasi ya shughuli za maendeleo zinazotekelezwa mkoani humo, zikiwemo zinazounganisha Tanzania Bara na Zanzibar kupitia sekta mbalimbali ikiwemo bandari.
“Fursa ya Muungano inatakiwa kusaidia pande zote, Bara na Zanzibar. Hili litasaidia zaidi sekta ya utalii kwani mtalii anapokuja Zanzibar anaweza kuunganisha safari yake na Bagamoyo pamoja na Hifadhi ya Saadani,” amesema.
Aidha, amewataka vijana kuwa makini na matumizi ya mitandao ya kijamii katika kipindi hiki cha utandawazi kutokana na kuwepo kwa upotoshaji unaofanywa na baadhi ya watu kupitia majukwaa hayo.
Amesema vijana wanapaswa kutumia mitandao ya kijamii kwa manufaa yao, hususan kujifunza mbinu za kuboresha shughuli za biashara ili kujikwamua kiuchumi.
Kwa upande wake, Mbunge wa Chalinze ambaye pia ni Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Ridhiwani Kikwete, amesema Chalinze inaendelea kubadilika kwa kasi kutokana na juhudi za Serikali kwa kushirikiana na wananchi.
Ameongeza kuwa ushirikiano mzuri kati ya viongozi na wananchi umeifanya Chalinze kuwa kivutio cha wawekezaji wengi kutokana na uwepo wa miundombinu rafiki, hali inayochochea ukuaji wa eneo hilo kila siku.
Awali, Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Abubakar Kunenge, alisema Wilaya ya Bagamoyo ni miongoni mwa maeneo ya utalii yanayokua kwa kasi kutokana na kuongezeka kwa wawekezaji wa ndani na nje wanaowekeza katika wilaya hiyo.
“Kuhusu suala la Muungano, hapa Pwani watu wengi kutoka Zanzibar na Bagamoyo hukutana na kufanya shughuli mbalimbali. Bagamoyo ni miongoni mwa maeneo ambayo wananchi wake wananufaika kwa kiasi kikubwa na Muungano wa nchi yetu,” amesema.
Kunenge amesema pia upo mpango wa kujenga reli ya kilomita 100 kutoka Bagamoyo hadi Bandari Kavu ya Kwala, ambao utarahisisha usafirishaji wa bidhaa mbalimbali kutoka eneo hilo.
Aidha, amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa ujenzi wa Barabara ya Afrika Mashariki pamoja na Barabara ya Mlandizi–Maneromango, ambazo amesema zitafungua fursa zaidi za usafirishaji na maendeleo ya uchumi.
Vilevile, amewataka wawekezaji kujenga hoteli kubwa za kitalii ili kuendana na ukuaji wa sekta ya utalii katika Wilaya ya Bagamoyo, ambayo kwa sasa ina fursa nyingi za maendeleo.
Mkuu huyo wa Mkoa pia amemuomba Waziri
Masauni kufikisha ombi la Halmashauri ya Chalinze kupandishwa hadhi na kuwa
Manispaa kutokana na kutimiza vigezo mbalimbali, ikiwemo ongezeko la mapato na
kasi ya maendeleo.

0 Maoni