Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais Dkt. Richard Muyungi amesema mabalozi wa mazingira wana nafasi kubwa katika kuisaidia nchi katika kuimarisha usimamizi wa mazingira.
Ametoa kauli hiyo alipokutana na mabalozi wa mazingira katika ukumbi wa Ofisi ya Makamu wa Rais jijini Dodoma kwa lengo la kujadili na kuweka mikakati ya usimamizi endelevu wa mazingira.
Akizungumza na mabalozi hao, Dkt. Muyungi pamoja na kuwapongeza kwa kazi nzuri ya kujitoa aliwahimiza kuendelea kuendelea kushirikiana na Serikali katika utekelezaji wa mikatati yake ikiwemo katika utekelezaji wa Dira 2050 hususan upandaji wa miti bilioni 10 ifikapo mwaka 2030.
Aliwaomba mabalozi hao wa mazingira waendelee kuhamasisha wananchi katika maeneo yao kushiriki kikamilifu katika zoezi la kukijanisha Tanzania kwa kupanda miti na kuitunza ili kunusuru kuenea kwa jangwa.
“Usimamizi wa vyanzo vya maji katika mabonde yetu ni muhimu ili tupate nishati yote haya hatuwezi bila ninyi mabalozi kushiriki katika kuhamasisha jamii ambayo mko nayo katika maeneo yenu, tuendelee kushirikiana,” alisema Dkt. Muyungi.
Aidha, Katibu Mkuu huyo alibainisha kuwa ni asilimia 37 ya taka zote hukusanya na kuchakatwa hivyo ni wakati sasa kwa kushirikiana na mabalozi wa mazingira kuhakikisha usimamizi wa taka unaimarika na kufikisha asilimia 100.
Halikadhalika,
alieleza kuwa mabalozi wa mazingira wawe chachu ya kuelimisha na kuhamasisha
jamii katika matumizi ya nishati safi ya kupikia ambayo Serikali imeweka lengo
kuwa ifikapo mwaka 2030 asilimia 80 ya wananchi wawe wanatumia.
“Tunapohimiza nishati safi tunahimiza pia kuondokana na umasikini na uharibifu wa mazingira pamoja na kutoa fursa kenye makundi ya wanawake na wasichana ili waende shule badala ya kutumia muda wao kwenda porini na kukata kuni,“ alisisitiza.
Sanjari na hilo alisema katika utunzaji wa mazingira kupitia misitu baada ya upandaji wa miti kuna fursa ya biashara ya kaboni hivyo alitoa rai kwa mabalozi wa mazingira kuwa mfano wa kushiriki katika biashara ya kaboni na kuachana na kasumba kuwa ni ya wageni pekee.
Katika
hatua nyingine, Dkt. Muyingi alikutana na kufanya mazungumzo
na ujumbe kutoka Shirika la BRAC Maendeleo Tanzania kwa lengo la kuimarisha ushirikiano katika utekelezaji wa shughuli mbalimbali
za maendeleo.
Katika mazungumzo hayo, pande zote mbili
zilijadili fursa za kupanua ushirikiano katika utekelezaji wa mradi mpya
unaojulikana kama BIGBET—programu ya kukabiliana na athari za mabadiliko ya
tabianchi.
Mradi huo unalenga kuwawezesha wanawake kujenga
ustahimilivu na kuwaondoa katika mazingira ya hatari yanayosababishwa na
mabadiliko ya tabianchi na ukitarajiwa kutekelezwa na BRAC Maendeleo Tanzania
kwa ushirikiano na Serikali pamoja na wadau mbalimbali wa maendeleo katika nchi
nne, ukitarajiwa kuleta matokeo chanya na endelevu kwa jamii zinazolengwa.
Ujumbe huo uliongozwa na Mkurugenzi Mkuu Bw.
Joydeep Sinha, akiambatana na Meneja wa Mradi Bw. Jumanne Magese na Naibu
Meneja wa Uhamasishaji wa Rasilimali Kelvin Edward.


0 Maoni