Dkt. Muyungi awataka wananchi kuitunza miradi ya maendeleo

  

Katibu Mkuu wa Ofisi ya Makamu wa Rais Dkt. Richard Muyungi ametoa rai kwa wananchi kuunga mkono jitihada za Serikali katika usimamizi endelevu wa mazingira kwa kuitunza miradi ya maendeleo inayotekelezwa katika maeneo yao. 

Ametoa wito huo wakati alipofanya ziara ya kutembelea na kukagua miradi mbalimbali ya maendeleo katika Wilaya ya Nyasa mkoani Ruvuma Julai 16, 2026. 

Akizungumza kwa nyakati tofauti wakati wa ziara hiyo, Dkt. Muyungi alisisitiza kuwa mazingira ndio uhai wa mwanadamu na ni sehemu ya uchumi kupitia fursa mbalimbali zinazopatikana katika sekta hiyo. 

“Ndugu zangu niwaombe tuhakikishe taifa letu tunalipeleka mbele hasa katika kutimiza ndoto ya kuwa na taifa lenye uchumi ulioimarika na hivyo kuweza kusonga mbele na kuleta manufaa,“ alisema. 

Katika ziara hiyo, miongoni mwa miradi aliyokagua Katibu Mkuu ni pamoja na mradi wa kizimba cha ufugaji wa samaki kilichopo katika Kijiji cha Hinga ambao utasaidia kupanuka wigo wa uvuvi hivyo kuchochea sekta ya uchumi wa buluu. 

Pia, mradi huo unatarajiwa kuwezesha ufugaji wa samaki kuanzia idadi ya 15,000 hadi 21,000 ambao ni wastani wa samaki tani nne baada ya miezi sita hivyo kuongeza kipato cha wafugaji na halmashauri hiyo kwa ujumla. 

Mradi mwingine aliotembelea Dkt. Muyungi ni ujenzi wa bandari ya Mbamba Bay ambaa ukikamilika utaunganishwa na bandari ya Mtwara kwa ajili ya kusafirisha mizigo kwenda nchi jirani. 

Faida nyingine ni kuwa makao makuu yaa bandari ya Nyasa yatahamishiwa bandari ya Mbamba Bay baada ya kukamilika kwa mradi na hivyo kuongeza mapato ya Serikali. 

Akizungumza mara baada ya kutembelea miradi hiyo kwa nyakati tofauti Katibu Mkuu Dkt. Muyungi alisema itakuwa ni chachu katika kuleta mabadiliko makubwa ya kiuchumi nchini Tanzania. 

Alisema kuwa Ofisi ya Makamu wa Rais ina kazi ya kusimamia mazingira na kuratibu masuala yanayohusu kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi ambayo inaathiri vyanzo vya maji yakiwemo maziwa kwa maji kujaa au kupungua. 

Kutokana na athari hizo, Dkt. Muyungi alisisitiza kuwa ni vyema miundombinu ya miradi inayojengwa ikazingatia uwezo wa kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi ambapo alitolea mfano ukuta wa Ocean Road (Barabara ya Obama) uliopo jijini Dar es Salaam ni mojawapo ya miundombinu iliyojengwa kwa ajili ya kuzuia mawimbi ya bahari yasiathiri eneo la nchi kavu.



 

Chapisha Maoni

0 Maoni