KAMISHNA
wa Maadili wa Tume ya Maadili ya Viongozi wa Umma, Jaji Sivangilwa
Mwangesi, amevitaka vyombo vya habari nchini kuendelea kushirikiana
na Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma katika kukuza uadilifu
na uwajibikaji miongoni mwa viongozi wa umma, akisisitiza kuwa jukumu
hilo linahitaji ushiriki wa wadau mbalimbali wakiwemo wahariri na
wanahabari.
Katika hotuba yake iliyosomwa na Kaimu Kamisha wa
Maadili Kassim Mkwawa katika Kikao na Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF) Jaji Mwangesi alisema ushirikiano kati ya
Sekretarieti ya Maadili na vyombo vya habari umeendelea kuzaa matunda
kwa miaka minne iliyopita, kupitia utoaji wa elimu kuhusu Sheria ya
Maadili ya Viongozi wa Umma Na. 13 ya mwaka 1995 na kubadilishana
mawazo yanayosaidia kuimarisha uadilifu nchini.
Alisema katika
mwaka wa fedha 2025/26 unaokaribia kumalizika, Sekretarieti hiyo
imefanya ziara katika kanda zake nane kwa lengo la kukutana na
wahariri wa maeneo mbalimbali na kujadili namna bora ya kuendeleza
ushirikiano katika kukuza maadili ya viongozi wa umma, huku
akiwapongeza wahariri kwa mchango wao katika kuibua mijadala chanya
inayolenga kuimarisha uwajibikaji.
Jaji Mwangesi alisema
Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma ilianzishwa kwa mujibu wa
Ibara ya 132 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka
1977 na Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma Na. 13 ya mwaka 1995,
huku akieleza kuwa taasisi hiyo ina jukumu la kutoa elimu ya maadili
kwa umma kupitia vyombo vya habari, semina, makongamano, maonesho na
mikutano mbalimbali.
Aidha, aliwataka wahariri na wanahabari kutumia taaluma yao katika kuibua na kuripoti masuala yanayohusu ukiukwaji wa maadili ya viongozi wa umma, akibainisha kuwa zipo njia mbalimbali zinazoweza kutumika kuwasilisha taarifa hizo ikiwemo barua pepe, mfumo wa mrejesho wa kielektroniki na simu, huku akisisitiza kuwa kazi ya kujenga uadilifu ni jukumu la kila Mtanzania.
Alisema kuwa uwepo wa viongozi waadilifu una manufaa makubwa kwa Taifa na vizazi vijavyo kwa kuhakikisha rasilimali za nchi zinawanufaisha wananchi wote, na kuwataka wahariri kuendelea kutumia kalamu na sauti zao kujenga umoja, mshikamano na kudumisha amani nchini, huku akivipongeza vyombo vya habari kwa kuendelea kuzingatia weledi na maadili ya taaluma katika kulinda maadili ya Mtanzania licha ya changamoto za utandawazi.
Kwa upande wa Wahariri wametaka maboresho kwenye sheria iweze kuruhusu mali za viongozi wa serikali kuwekwa hadharani kwenye mitandao ya kijamii ili kila mmoja ajue anachokimiliki kiongozi wake.
Akizungumza katika kikoa hicho jijini Da es Salaam Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF) Deodatus Balile, amesema ifike hatua mali za viongozi ziweke hadharani akisema hatua hiyo itasaidia kuondoa minongono ya wananchi dhidi ya viongozi.
Katibu wa Idara ya Ukuzaji Maadili ya Viongozi wa Umma, Waziri Kipacha, amesema sheria ya maadili ya viongozi wa umma na kanuni zake, hasa ya tamko la rasilimali, maslahi na madeni imeweka utaratibu wa wananchi kukagua taarifa za mali za viongozi.
Katibu Usimamizi wa Maadili kutoka Ofisi ya Rais, Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma, Kassim Mkwawa, amesema malalamiko ni mengi lakini hatua wanayoichukua ni kuyafanyia kazi.
“Lakini tunapofanya uchunguzi hua hatusemi, uchunguzi ni siri, hadi hapo itakapolazimika kusema, japo kuna haja kubwa ya kuelimisha jamii kuhusu taratibu za kisheria,” amesema.



0 Maoni