Waziri wa Madini, Mheshimiwa Anthony Mavunde (Mb) ameielekeza Timu ya Majadiliano ya Serikali kwenye Sekta ya Madini (GNT) kuwaita na kufanya nao majadiliano wamiliki wote wa leseni za uchimbaji madini kinywe nchini Tanzania kujadiliana kuhusu ubia wa serikali katika Kampuni hizo na kuwataka kuanza utekelezaji wa uchimbaji kwa mujibu wa masharti ya leseni na Sheria ya Madini Sura ya 123.
Ameyasema
hayo leo tarehe 30 Mei, 2026 Wilayani Ruangwa aliposhiriki zoezi la
utiaji saini na Kampuni za Grafica Resources na Eminent Minerals
Limited zenye ubia wa uwekezaji wa hisa asilimia 83 na Serikali
asilimia 17 kwa kila kampuni.
"Sisi sekta ya madini
tunamshukuru kwa dhati Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa namna
anavyotupa maelekezo na kutuwezesha kusimamia sekta kikamilifu kwa
maendeleo ya Taifa letu"
"Na ndiyo maana Kampuni
zote ambazo hazijaanza uzalishaji kwa mujibu wa masharti ya leseni
zao tumeziandikia hati ya makosa (Default Notice) kwa mujibu wa
Sheria ya Madini Sura ya 123. Kusaini kwetu mikataba siku ya leo,
hakutoi unafuu kwa wawekezaji hawa kutotekeleza uwekezaji wao kwa
mujibu wa Sheria yetu ya madini" amesisitiza Mhe.
Mavunde.
Waziri Mavunde amesema hatua ya Timu ya GNT kuwaita
na kuwataka wamiliki wa leseni za uchimbaji madini kinywe kufuata
masharti ya Sheria na kuanza uzalishaji kutapelekea ufikiaji wa lengo
la kuifanya Tanzania kuwa mzalishaji wa kwanza duniani wa madini
kinywe ifikapo mwaka 2030.
Vilevile, Waziri Mavunde ametoa
wito kwa wawekezaji wa miradi hiyo kutoa fursa ya kipaumbele cha
ajira kwa watanzania hususan wanaozunguka miradi hiyo. Kwa kufanya
hivyo kutachochea uchumi wa Vijiji, Wilaya ya Ruangwa hususan kupitia
wajibu wa uwekezaji kwa jamii (CSR) na kupelekea maendeleo ya uchumi
wa Nchi yetu.
Aidha, Waziri Mavunde amebainisha kuwa miradi
hiyo itakapoanza kuzalisha kikamilifu, itakuwa na uwezo wa kuzalisha
tani 101,048 za kinywe kila mwaka kwa upande wa mradi wa Grafica na
tani 15,930 za kinywe kila mwaka kwa upande wa mradi wa Eminent
mtawalia, hali inayoifanya Ruangwa sasa kuwa sehemu ya mnyororo wa
thamani wa teknolojia za kisasa duniani.
Waziri Mavunde pia
ameeleza kuwa bado Tanzania ina nafasi kubwa ya kufanya vizuri katika
uzalishaji wa madini mbalimbali duniani, na ndiyo maana tunaendelea
kuweka mkazo kwenye ufanyaji wa utafiti wa kina ili kubaini mashapo
zaidi yatakayoongeza uchimbaji hususan kupitia wachimbaji wadogo
wenye mchango mkubwa katika uchumi wetu.
Awali, akieleza
mchakato wa kufikia makubaliano hayo, Mwenyekiti wa Timu ya
Majadiliano ya Serikali kwenye sekta ya Madini, Prof. Sifuni Mchome
amebainisha kuwa, majadiliano hayo yalifanyika kwa kuzingatia maslahi
mapana ya nchi yetu na hayakuwa na lengo la kutafuta mshindi, hali
iliyopelekea Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupata hisa
zisizofifishwa za asilimia 17 kwenye kila mradi wa ubia.
Kwa
upande wake, Mkurugenzi wa Kampuni ya Grafica Resources, Bw. Vikas
Bardiya ameeleza kuwa kampuni yao inaishukuru Serikali kwa
ushirikiano iliyowapa mpaka kufikia makubaliano ya kuwekeza na
kuahidi kwamba watahakikisha wanatekeleza uwekezaji huo kwa mujibu wa
mkataba ili uweze kuleta manufaa kwa wananchi wa Ruangwa na Taifa kwa
ujumla.
Pia, Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Eminent
Minerals Limited, Bw. Shafiqali Khaki ameeleza kufarijika kwao kuwa
kampuni ya kizawa kuingia ubia na Serikali katika uwekezaji kwenye
mradi huo wa uchimbaji madini kinywe na kwamba wao kama wazawa
watahakikisha sehemu kubwa ya zaidi ya ajira 250 zitakazozalishwa
katika uwekezaji huo zinachukuliwa na watanzania ili kuinua uchumi wa
Taifa letu.
Naye Mkuu wa Mkoa wa Lindi, Mheshimiwa Zainab
Telack alimshukuru Mhe. Rais kwa kuwa kiongozi mahiri katika
kusimamia uchumi na kuhakikisha rasilimali zetu zinanufaisha
watanzania. Aidha, alisisitiza kuwa Serikali ya Mkoa wa Lindi
itaendelea kuwapa ushirikiano wawekezaji hao ili waweze kuendesha
shughuli zao kwa kasi na kunufaisha wananchi wa Lindi na Taifa kwa
ujumla.


0 Maoni