Na. Edmund Salaho - Dodoma
Waziri wa Maliasili na Utalii
Mhe. Ashatu Kijaji leo Mei, 15 2026 amebainisha kete nne muhimu
zitakazotumiwa na Wizara ya Maliasili na Utalii na taasisi zake ili
kufikia lengo la watalii millioni nane (8) ifikapo mwaka 2030 pamoja
na kuongeza mchango wa Sekta ya Utalii katika pato la Taifa kutoka
asilimia 17 mwaka 2025 hadi asilimia 20 mwaka 2030.
Akiwasilisha
makadirio ya bajeti ya Wizara ya Maliasili na Utalii Bungeni, jijini
Dodoma Waziri Kijaji alitaja kete hizo ambazo Wizara imejipanga
vilivyo kutumia ili kuongeza idadi ya watalii katika maeneo ya
vivutio nchini kuwa ni matukio ya Kimataifa yatakayofanyika nchini.
“Wizara itaendelea kutumia fursa na mikakati mbalimbali ya
kukuza utalii kupitia matukio ya kimataifa kama Mashindano ya Mpira
wa Miguu kwa Nchi za Afrika (Africa Cup of Nations - AFCON) 2027,
Shindano la 74 la Ulimbwende wa Dunia 2027 - Miss World 2027, Mkutano
wa 153 wa Umoja wa Mabunge Duniani (Inter-Parliamentary Union (IPU)
Assembly) Tukio la World Travel Awards (WTA) 2026 ambayo yote
yanatarajiwa kufanyika nchini ” alisema Waziri Kijaji
Mkutano
wa Umoja wa Mabunge duniani unakutanisha Mabunge ya Nchi wanachama wa
umoja wa mabunge Duniani na utafanyika mwanzoni mwa Oktoba mwaka huu
2026 Jijini, Arusha unatarajiwa kuwa na washiriki zaidi ya 1,500
wakiwemo Maspika 183 kutoka nchi mbalimbali duniani ambapo Tanzania
ni mwanachama na mwenyekiti wa umoja huo.
“Na kuongeza kuwa
Tukio la kimataifa tuzo za ubora katika Sekta ya Utalii duniani
(World Travel Awards (WTA) 2026) linatarajiwa kufanyika nchini mwezi
Desemba, 2026 nchini linatarajiwa kuhudhuriwa na washiriki zaidi ya
1,000 kutoka Mabara ya Afrika, Ulaya, Asia, Amerika ya Kaskazini na
Kusini, huku Shindano la 74 la Ulimbwende wa Dunia 2027 (Miss World
2027) likiwa ni miongoni mwa mashindano makubwa duniani
yanayojulikana kama Big Four Beauty Pageants linatarajiwa kufanyika
nchini mwezi Mei, 2027 na linatarajiwa kuhudhuriwa na watu takriban
20,000 wakiwemo washindani 120 kutoka nchi mbalimbali Duniani”.
Aidha, Waziri Kijaji aliongeza kuwa kete nyingine ni Mashindano
ya AFCON 2027 yanayoandaliwa na Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika
(CAF) yanatarajiwa kufanyika kwa pamoja katika nchi za Afrika
Mashariki ikiwemo Tanzania. Mashindano hayo yatahusisha timu 24
kutoka mataifa mbalimbali ya Afrika na yanatarajiwa kuvutia zaidi ya
watazamaji milioni 1.8 viwanjani pamoja na watazamaji wa televisheni
bilioni 1.9 duniani kote kupitia vituo zaidi ya 185 vya utangazaji na
yanakadiriwa kuzalisha faida za kiuchumi zinazoweza kufikia zaidi ya
Dola za Marekani bilioni 2.
Wizara pia imeandaa mkakati
maalum wa kuitangaza Tanzania kama kivutio cha kipekee cha utalii
kabla na baada ya mashindano ya Kombe la dunia kwa kuandaa kampeni za
kimataifa za utangazaji kupitia Mashindano ya Kombe la Dunia la FIFA
2026 yatakayofanyika nchini Marekani, kwa kushirikisha wadau na
mbalimbali wakiwemo watangazaji maarufu wa michezo, watu wenye
ushawishi mkubwa pamoja na matumizi ya majukwaa ya kidijitali na
mabango katika maeneo ya kimkakati.


0 Maoni