Wagombea wa nafasi ya urais katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025 wamemmwagia sifa na pongezi nyingi Rais Samia Suluhu Hassan kufuatia uamuzi wake wa kuunda Tume ya Uchunguzi wa Kijinai wa Matukio ya Wakati na Baada ya Uchaguzi Mkuu.
Hatua
hiyo ya rais imekuja ikiwa ni utekelezaji wa haraka wa mapendekezo
yaliyotolewa na Tume ya Kuchunguza Matukio Wakati na Baada ya
Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 2025 iliyokuwa chini ya Jaji Mkuu Mstaafu
Mohamed Chande Othman.
Viongozi hao wamempongeza Rais Samia
kwa kuonyesha nia thabiti ya kuliponya taifa kwa kutumia Sheria ya
Tume za Uchunguzi kuunda chombo hicho maalum kitakachoshughulikia
viashiria vyote vya jinai vilivyobainika.
Miongoni mwa
waliotoa pongezi hizo ni aliyekuwa mgombea urais kupitia chama cha
Makini, Coster Kibonde, aliyempongeza rais kwa weledi mkubwa
alioonyesha katika kuteua majaji wastaafu na wabobezi wa sheria
nchini, akiamini kuwa uteuzi huo unaenda kumaliza 'kiporo' cha
kipelelezi kilichoachwa na ripoti ya kwanza.
Pongezi hizo
ziliungwa mkono na aliyekuwa mgombea urais kupitia Chama cha Wakulima
(AAFP), Kunje Ngombale Mwiru, aliyesifu uamuzi huo akieleza kuwa
kuundwa kwa tume hiyo ni jambo jema linalolenga kuweka uwiano mzuri
wa mwenendo wa usalama wa taifa. Viongozi hao wamebainisha kuwa
uamuzi wa rais kuweka hadharani ukweli utasaidia kwa kiasi kikubwa
kutibu majeraha ya Oktoba 29 na kuimarisha msingi wa maridhiano ya
kitaifa.

0 Maoni