Serikali imeiwezesha
Wakala ya Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) kupata dola milioni
65 kwa ajili ya utekelezaji wa matengenezo ya miundombinu ya barabara
kupitia mfuko wa dharura (CERC).
Hayo yamesemwa na Mtendaji
Mkuu wa TARURA, Mhandisi Victor Seff wakati wa ziara ya wajumbe wa
Bodi ya Ushauri ya Wakala huo katika mradi wa ujenzi wa daraja lenye
urefu wa Mita 22 pamoja na barabara za maingilio zenye urefu wa Mita
290 kwenye barabara ya Ndovelwa yenye urefu wa Km. 20.2 katika
Manispaa ya Tabora.
Mhandisi Seff amesema fedha hizo ni mkopo
nafuu kutoka Benki ya Dunia uliotolewa kufuatia tathmini ya uharibifu
wa miundombinu uliosababishwa na mvua za El-Nino za mwaka
2024.
Amesema tathmini hiyo ilibaini maeneo mengi ya barabara
yaliyoharibiwa na hivyo kuhitaji matengenezo ya haraka ili kurejesha
mawasiliano na huduma kwa wananchi.
“Miradi hii inatekelezwa
nchi nzima na kwa wastani utekelezaji wake umefikia asilimia 70. Kazi
zote zinatarajiwa kukamilika ifikapo Septemba 2026,”
Alisema.
Aidha, amesema miradi hiyo inatekelezwa na
makandarasi wazawa huku akiwasisitiza Mameneja na wasimamizi wa
TARURA nchini kuongeza usimamizi ili kuhakikisha miradi inakamilika
kwa viwango vinavyotakiwa.
Akizungumzia ujenzi wa daraja hilo,
Mhandisi Seff amesema ameridhishwa na ubora wa kazi inayoendelea na
kusisitiza kuwa miundombinu inayojengwa inapaswa kudumu na kupitika
wakati wote ili kuwawezesha wananchi kufikia masoko, shule na
kusafirisha pembejeo za kilimo.
Kwa upande wake, Makamu
Mwenyekiti wa Bodi ya Ushauri ya TARURA Bi. Nunu Mangu amesema
ujenzi wa daraja na barabara hizo utasaidia kufungua mawasiliano kwa
wananchi wa maeneo husika na kuhakikisha usafiri unakuwa wa uhakika
katika misimu yote ya mwaka.
Pia aliwataka wananchi kuitunza
miundombinu inayojengwa kwa kuwa Serikali kupitia TARURA inaendelea
kuwekeza fedha nyingi kuboresha miundombinu nchini.



0 Maoni