WAZIRI
MKUU, Dkt. Mwigulu Nchemba amesema Serikali inapanga kufanya
maboresho katika mfumo wa stakabadhi ghalani ili kuondoa changamoto
zinazowakabili wakulima hususan gharama na usumbufu wa kufuata huduma
za maghala yaliyo mbali na maeneo yao ya uzalishaji.
Amesema
hayo leo Jumamosi, Mei 16, 2026 wakati akizungumza na wananchi wa
Kata ya Mnenia, Halmashauri ya Wilaya ya Kondoa mkoani Dodoma katika
mwendelezo wa ziara yake ya kusikiliza na kutatua changamoto za
wananchi.
Waziri Mkuu amesema Serikali imepokea malalamiko
mbalimbali kuhusu utekelezaji wa mfumo huo na kwamba hatua
zinaendelea kuchukuliwa ili kuhakikisha mfumo huo unawanufaisha
wakulima kama ilivyokusudiwa.
“Maelekezo ya Ilani ya
Uchaguzi ni wananchi wasiyafuate maghala, maghala yawafuate wananchi
pale walipo,” amesema.
Aidha, Waziri Mkuu amesema ataitisha
kikao maalumu kitakachowahusisha wakuu wa mikoa pamoja na sekta
zinazohusika kutoka maeneo yanayozalisha mazao yanayotumia mfumo wa
stakabadhi ghalani ili kufanya tathmini ya changamoto zilizopo na
namna ya kuzitatua.
“Nitaitisha kikao cha wakuu wa mikoa ya
maeneo haya yanayozalisha mazao ambayo wananchi wake wamekuwa
wakipata changamoto ili tupate mpango kazi wa namna ya kumaliza
tatizo hili,” amesema.
Ametaja baadhi ya mikoa inayohusika
kuwa ni Dodoma, Singida, Simiyu, Tabora pamoja na baadhi ya mikoa ya
Kusini inayozalisha mazao ya biashara ikiwemo ufuta na dengu.
Katika
hatua nyingine, Waziri Mkuu amesema Serikali imeelekeza wanunuzi wa
mazao kutumia taasisi za kifedha kupata mikopo badala ya kuwakopesha
wakulima kabla ya mauzo ya mazao yao.
“Wenzetu wanaokwenda
kununua haya mazao wasiwakope wakulima, wao wakakope benki. Benki
ndiyo taasisi zinazotoa mikopo,” amesema.
Amesema Serikali
itaendelea kufuatilia utekelezaji wa mfumo huo ili kuhakikisha
wakulima wanapata huduma kwa urahisi na kunufaika ipasavyo na mazao
yao.


0 Maoni