Ushirikishwaji hafifu na hisia za kutosikilizwa
zimetajwa kuwa miongoni mwa vichocheo vilivyowafanya baadhi ya vijana
kujitenga na mifumo halali ya kidemokrasia na kujiingiza kwenye
propaganda wakati wa Uchaguzi Mkuu wa 2025.
Hilo limebainika
kupitia Ripoti ya Tume ya Jaji Mohamed Chande Othman, ambayo
imesisitiza haja ya kujenga mifumo mipya ya kusikiliza sauti za
vijana mapema.
Ripoti inaeleza kuwa vijana wengi waliohojiwa
walionesha hisia za kutokuwakilishwa kikamilifu katika mijadala
mikubwa ya kisiasa na kijamii, jambo lililowafanya baadhi yao kuamini
kaulimbiu za 'mabadiliko' ya vurugu kupitia mitandao ya kijamii.
Ili kurekebisha hali hii, tume imependekeza kuwepo kwa
mikakati madhubuti ya kutoa elimu ya uraia ili kujenga kizazi
kinachoweza kuchambuzi taarifa kwa umakini na kushiriki siasa kwa
njia za amani.
Hata hivyo, Jaji Chande aligusia kuwa wananchi
na vijana wengi waliofika mbele ya tume hiyo bado wana matumaini
makubwa na mustakabali wa Tanzania, wakitamani kuona taifa linarudi
kwenye misingi ya amani, umoja na mshikamano.
Ili kufikia
lengo hilo, ripoti imetoa wito wa kuongezwa kwa nafasi za vijana
katika uongozi, ubunifu, na mijadala ya sera ili wawe nguzo ya
maendeleo badala ya kuwa chombo cha migogoro.

0 Maoni