Na Beda Msimbe, BSKY Media
Tanzania imefanikiwa kujijenga kama taifa imara, lenye mshikamano na umoja thabiti katika kipindi cha miongo sita iliyopita, huku ikisisitizwa kuwa ni taifa kamili na si mkusanyiko wa makabila kama yalivyo mataifa mengine mengi barani Afrika.
Kauli hiyo imetolewa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Uratibu na Wenye Ulemavu, Profesa Palamagamba John Aidan Mwaluko Kabudi, wakati akizungumza kwenye kongamano kubwa la wanafunzi wa vyuo vikuu lililoandaliwa na Jumuiya ya Wanafunzi wa Vyuo na Vyuo Vikuu (TAHLISO) jijini Dar es Salaam.
Akihutubia katika kongamano hilo Profesa Kabudi alieleza kuwa maisha ya mwanadamu ni hatua na ni muhimu mno kwa vijana kuijua jana yao, historia ya nchi yao, elimu ya uraia na uzalendo ili kutambua walipo na wanakoelekea bila kupata shida ya kupoteza mwelekeo.
Katika kufafanua upekee wa Tanzania, Profesa Kabudi alibainisha kuwa nchi ikiwa na zaidi ya makabila 125 yanayoelewana na kuishi kwa amani yakijumuisha makundi makuu yote ya kiasili barani Afrika ambayo ni Wabantu, Wanilotes kama Wajaluo na Wamasai, Watatoga, Wabarbaigi, na Wakushi kama Wairaqw, huku Wasandawe wakiwakilisha Wakhoisan.
Alitolea mfano kuwa nchi kama Nigeria ina makabila mengi lakini yote ni ya asili ya Kibantu, wakati Tanzania imekusanya makundi yote haya tofauti na kufanikiwa kuyaungamanisha kuwa taifa moja linalozungumza lugha moja na lenye utulivu mkubwa wa kijamii na kisiasa.
Aliongeza kuwa mbali na utofauti wa kikabila, Tanzania ni taifa ambalo halina dini kikatiba lakini wananchi wake wana dini na imani tofauti ambao wamefanikiwa kuishi kwa kuvumiliana na kuheshimiana, jambo linaloifanya nchi hiyo kuwa mfano wa kuigwa barani Afrika kwa kuwa na utengamano thabiti wa kijamii bila kubaguana.
Profesa Kabudi alieleza kuwa dhana ya "Never Again" (Asilani Isitokee Tena) ni msukumo mkubwa wa kulinda amani na mshikamano na ni ahadi ya kutokubali kurudishwa nyuma kiwango cha kutoheshimu misingi ya nchi kikatiba, ambapo ibara ya tatu inatamka wazi kuwa Tanzania ni nchi ya kidemokrasia na ujamaa.
Aliipitisha hadhira hiyo kwenye historia ya kidemokrasia tangu uchaguzi wa kwanza wa kuelekea uhuru mwaka 1958, hadi mabadiliko ya mwaka 1964 yaliyofuatia mapendekezo ya Tume ya Kambona yaliyoifanya nchi kuendeshwa kwa mfumo wa chama kimoja hadi mwaka 1992 mifumo ya vyama vingi iliporejeshwa.
Waziri huyo aliwakumbusha vijana kuwa Tanzania imepita katika dhoruba na nyakati nzito sana za kihistoria ikiwemo uasi wa wanajeshi wa mwaka 1964, kuvunjika kwa Jumuiya ya Afrika Mashariki mwaka 1977 kulikoilazimisha nchi kuanza upya kiuchumi, Vita vya Kagera dhidi ya Uganda mwaka 1978, pamoja na kesi kubwa za uhaini za miaka ya 1970 na 1982, lakini yote hayo yalishindwa kuigawa nchi kwa sababu ya uzalendo mkubwa wa wananchi na mapenzi yao kwa taifa lao.
Suala la ulinzi wa taifa pia lilipewa uzito mkubwa ambapo Profesa Kabudi alifafanua kwa mujibu wa Katiba, ibara ya nane na ya tisa, kuwa jukumu la ulinzi na usalama si la serikali au vyombo vya dola pekee bali ni wajibu wa kila mwananchi. Alitolea mfano wa kihistoria ambapo mwaka 1971 kuanzishwa kwa Jeshi la Mgambo kulilenga kuwashirikisha wananchi wenyewe, na mgambo hao walikuja kuwa msaada mkubwa sana katika kupigana Vita vya Kagera mwaka 1978 baada ya nchi kuvamiwa.
Aligusia pia maamuzi magumu ya kidiplomasia yaliyochukuliwa huko nyuma kutokana na misingi ya nchi kama vile kuvunja uhusiano na Uingereza mwaka 1965 kulikosababisha nchi kukosa msaada wa kifedha, kuvunja uhusiano na Ujerumani ya Magharibi (Bonn) mwaka 1964, na uamuzi wa Mwalimu Julius Nyerere wa kufunga mpaka na Kenya mwaka 1977, akisisitiza kuwa mambo yote magumu yaliyowahi kufikiriwa tayari yameshatokea huko nyuma lakini nchi ilisimama imara.
Katika kueleza mchango mkubwa wa Tanzania kimataifa, Profesa Kabudi aliunga mkono kauli ya Rais wa Uganda, Yoweri Museveni, aliyewahi kusema kuwa katika ulimwengu wa sasa hakuna kiongozi anayemfikia Mwalimu Julius Nyerere kwa kuwa Tanzania ilikuwa tayari kujitoa mhanga na kupoteza rasilimali zake chache kwa ajili ya kukomboa mataifa mengine.
Alifafanua kuwa nchi haikufaidi "utoto" wake kwani ilipigania uhuru wa nchi za Kenya, Uganda, Msumbiji, Zimbabwe, Afrika Kusini na DRC, ambapo hata baada ya kuuawa kwa Waziri Mkuu wa kwanza wa DRC, Patrice Lumumba, Tanzania ilisimama kidete kutoka Mwanzo kusaidia jirani zake, jambo linalofanya Rais Museveni kuwakumbusha raia wa Uganda (Abazukuru-wajukuu) wasiisahau kamwe Tanzania kwani bila mchango wake nchi hiyo isingefika ilipo leo.
Kuhusu maendeleo ya sasa, Profesa Kabudi alionyesha kuwa msimamo wa "Never Again" unamaanisha pia kuunga mkono juhudi za Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan katika kuwaletea wananchi ustawi, akitolea mfano ukamilishaji wa miradi mikubwa kama Bwawa la Kufua Umeme la Julius Nyerere (JNHPP) lenye visiwa sita ndani yake, urefu wa kilomita 100 na upana wa kilomita 25, mradi ambao ulifikiriwa tangu enzi za Mwalimu Nyerere na sasa umewezesha umeme kufika vijiji vyote na kupelekwa kwenye vitongoji, jambo linaloshangaza watu wa nje ya nchi.
Vilevile alieleza mapinduzi makubwa yanayofanyika kwenye sekta ya elimu chini ya Rais Samia, akibainisha kuwa tofauti na wakati nchi inapata uhuru ikiwa haina chuo kikuu hata kimoja, kwa sasa kuna vyuo vingi vilivyosambaa nchi nzima na uwepo wa Bodi ya Mikopo umesaidia kuzalisha wasomi wengi.
Alizungumzia pia mabadiliko ya kihistoria katika mfumo wa elimu ambapo kuanzia mwaka 2028, elimu ya msingi nchini Tanzania itakuwa hadi kidato cha nne (Form Four), ambapo shule zote za msingi zitakuwa na madarasa ya sekondari na zile za sekondari zitakuwa na madarasa ya awali na msingi, mabadiliko makubwa ambayo mara ya mwisho kufanyika ilikuwa mwaka 1967 wakati Mwalimu Nyerere alipoondoa shule za kati (Middle Schools) na kuweka darasa la kwanza hadi la saba.
Profesa Kabudi alisema maono ya sasa ya Rais Samia ni kuleta elimu ya amali (ushindani na ujuzi) ili kugeuza vyuo kuwa sehemu za kujenga uwezo unaojikita kwenye utendaji (competency-based knowledge) badala ya nadharia pekee, akitolea mfano wa mfumo wa Ujerumani ambapo wanafunzi wakimaliza sekondari ni lazima wachukue mwaka mzima wa mafunzo ya ufundi kabla ya kuendelea na mambo mengine.
Waziri Kabudi aliwasihi wanafunzi hao wa vyuo vikuu kulinda amani ya nchi kwa nguvu zote akionya kuwa mtu akiharibu Tanzania hana mahali pengine pa kwenda na huko kwingine atakuwa mkimbizi tu, huku akitoa wito wa kurejeshwa kwa utamaduni wa mdahalo (debates) katika taasisi za elimu.
Alieleza kuwa mijadala inasaidia watu kujenga hoja kwa unyenyekevu, kuongeza maarifa na kuwa wavumilivu kusikiliza mawazo ya wengine, na kuonya kuwa jamii isiyojifunza kujenga hoja kupitia midahalo hukimbilia matusi, kashfa na mipasho kwa kushindwa kuhimili nguvu ya hoja. Aidha vijana waliaswa kutambua kuwa wao ndio walinzi wakuu wa kesho ya Tanzania, na wanapaswa kusimama kidete kuzuia njama zozote zenye lengo la kuugawa mshikamano wa kitaifa.

0 Maoni