Mkurugenzi Mkuu wa TCAA amefanya kikao na Wadau wa Sekta ya Anga

 

Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania (TCAA), Dkt. Jabiri K. Bakari, tarehe 19 Mei 2026 alifanya vikao vya mashauriano na wadau wa sekta ya anga katika Makao Makuu ya TCAA yaliyopo Banana, Ukonga jijini Dar es Salaam.

Vikao hivyo vilifanyika katika vipindi viwili tofauti ambapo kikao cha asubuhi kilihusisha wamiliki na waendeshaji wa mashirika ya Ndege ya ndani, huku kikao cha mchana kikihusisha wamiliki na waendeshaji wa mashirika ya Ndege kutoka nje yanayokuja na kufanya shughuli zao nchini Tanzania.

Vikao hivyo vilitoa fursa kwa wadau kufanya majadiliano ya wazi na ya kujenga na uongozi wa TCAA, ambapo walitoa maoni, uzoefu na kueleza changamoto mbalimbali zinazoikabili sekta ya anga.

Akizungumza wakati wa ufunguzi wa vikao hivyo, Dkt. Bakari alijitambulisha rasmi kwa wadau na kusisitiza dhamira yake pamoja na menejimenti ya TCAA kuhakikisha sekta ya anga nchini inaendelea kufanya kazi kwa ufanisi na kukua zaidi.

Alieleza kuwa TCAA itaendelea kushirikiana kwa karibu na wadau wote wa sekta hiyo ili kuboresha utoaji wa huduma na kuimarisha maendeleo ya sekta ya anga nchini.

Dkt. Bakari pia aliwaeleza wadau kuwa TCAA ipo katika mchakato wa kuboresha na kuoanisha mifumo yake ili kurahisisha michakato ya biashara na kuongeza ufanisi wa huduma. Aliwataka wadau kuwa tayari kuunga mkono maboresho hayo pindi yatakapohitajika.

Aidha, alitangaza kuwa TCAA inapanga kuanzisha namba maalum ya bure ya simu pamoja na dawati maalum la huduma kwa Wateja ili kurahisisha mawasiliano na kushughulikia changamoto zao kwa haraka zaidi.

Katika majadiliano hayo, wadau waliwasilisha mapendekezo, maoni pamoja na changamoto mbalimbali zinazoathiri shughuli za sekta ya anga. Akijibu hoja hizo, Dkt. Bakari aliwahakikishia wadau kuwa TCAA imepokea na kuzingatia masuala yote yaliyowasilishwa na kwamba menejimenti ya mamlaka hiyo itashirikiana kwa karibu na wadau kuhakikisha changamoto hizo zinapatiwa ufumbuzi stahiki kwa ajili ya maendeleo endelevu ya sekta ya anga nchini Tanzania.

Akihitimisha vikao hivyo, Dkt. Bakari alisisitiza kuwa TCAA imejipanga kuhakikisha sekta ya anga nchini Tanzania inaendelea kukua, akieleza kuwa kama sekta ya anga inavyofanya kazi saa 24 kwa siku, vivyo hivyo TCAA ipo tayari kuwahudumia wadau wake wakati wote.

Vikao hivyo vya ushirikishwaji wa wadau vinaendelea.

Chapisha Maoni

0 Maoni