Rais mstaafu wa Awamu ya Nne Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete,
leo Mei 29, 2026 amekutana tena na Bi. Catherine P. Conrad Minja,
aliyefanyiwa upasuaji wa moyo kwa mafanikio akiwa na umri wa miaka
minne katika taasisi ya Muhimbili Orthopaedic Institute (MOI) miaka
18 iliyopita.
Wakati huo madaktari bingwa wa Moyo wa Taasisi
ya Moyo ya JKCI walikuwa wakitumia majengo ya MOI kabla jengo lao
halijakamilika.
Mara ya kwanza wawili hao walikutana Novemba
14, 2008 wakati Dkt. Kikwete akiwa Rais alipokwenda kumjulia hali
Catherine hapo MOI baada ya kufanyiwa upasuaji wa moyo mapema wiki
hiyo. Wakati huo Catherine alikuwa mmoja wa wagonjwa wa mwanzo
kufanyiwa upasuaji huo katika taasisi hiyo.
Miaka 18 baadaye,
Catherine amekua na sasa ni mwanafunzi wa mwaka wa kwanza wa Shahada
ya Udaktari katika Chuo Kikuu cha Kairuki jijini Dar es
salaam.
Alifika ofisini kwa Rais Mstaafu kumsabahi na
kumshukuru kwa mchango wake katika kuanzisha na kuimarisha huduma za
matibabu ya magonjwa ya moyo nchini.
Dkt. Kikwete alimpongeza
Catherine kwa kutimiza ndoto yake ya kusomea udaktari, jambo ambalo
aliahidi kulifanya alipokuwa mtoto. Alisema amefurahishwa kumuona
akiwa mwenye afya njema na akijiandaa kulitumikia taifa kupitia
taaluma ya tiba.
Kwa upande wake, Catherine alisema anatamani
kuwa Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Moyo ili kuwasaidia wagonjwa wenye
changamoto kama aliyowahi kupitia yeye mwenyewe, akieleza kuwa hiyo
itakuwa ni moja ya njia ya kumshukuru Mungu kwa zawadi ya maisha na
afya njema.


0 Maoni