Wilaya ya Ruangwa mkoani Lindi imeendelea
kushuhudia mageuzi makubwa ya kiuchumi na kijamii kufuatia kuongezeka
kwa shughuli za uchimbaji madini katika Mgodi wa Namungo unaomilikiwa
na kampuni ya Elianje Limited, huku wachimbaji wadogo na wananchi wa
maeneo yanayouzunguka mgodi huo wakinufaika kupitia ajira, biashara
na utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo.
Ukuaji wa
shughuli za uchimbaji katika mgodi huo umechangia kuboresha huduma za
maji, elimu, afya na miundombinu, hali iliyobadili maisha ya wananchi
ambao miaka michache iliyopita walikabiliwa na changamoto kubwa za
kiuchumi na kijamii.
Akizungumza kwa niaba ya Afisa Madini
Mkazi wa Lindi, Mhandisi Dickson Joram amesema hali ya wachimbaji na
wananchi wa Namungo imebadilika kwa kiwango kikubwa ikilinganishwa na
mwaka 2019 alipowasili katika eneo hilo.
Amesema wakati huo
shughuli za uchimbaji zilikuwa katika kiwango cha chini, huku
wachimbaji wengi wakitumia njia duni za uzalishaji na kushindwa
kumudu mahitaji muhimu ya kila siku.
“Wachimbaji wengi
walikuwa wanapitia kipindi kigumu sana. Ulipowatembelea ilibidi
wakati mwingine uwaachie fedha za chakula au kuwasaidia mahitaji
muhimu. Lakini leo Namungo imebadilika kwa kiasi kikubwa; wananchi
wanajitegemea na wanaendesha shughuli kubwa kupitia sekta ya madini,”
amesema.
Kwa upande wake, Afisa Uhusiano wa kampuni ya Elianje
Limited, Joseph Shayo amesema kampuni hiyo ilianza shughuli za
utafiti na uchimbaji mwaka 2020 na tangu wakati huo imekuwa
ikihakikisha jamii inayouzunguka mgodi inanufaika moja kwa moja
kupitia utekelezaji wa miradi ya kijamii.
Amesema kampuni
imefanikiwa kuchimba visima na kusambaza maji katika Kijiji cha
Tongwe na Kitongoji cha Namungo, huku maboresho ya huduma hiyo
yakiendelea katika maeneo yenye changamoto ya upatikanaji wa maji
safi na salama.
Mbali na huduma ya maji, amesema kampuni
imejenga shule ya awali, kuboresha madarasa, kujenga vyoo vya kisasa
pamoja na kushiriki katika ujenzi wa shule ya msingi katika Kitongoji
cha Namungo ili kupunguza adha ya watoto kutembea umbali mrefu
kufuata huduma za elimu.
Shayo amesema mgodi huo pia
umechangia uboreshaji wa barabara zinazounganisha vijiji na kata
jirani sambamba na kusaidia shule mbalimbali kwa kutoa vifaa vya
elimu ikiwemo kompyuta na mashine za uchapishaji.
Naye
Mwenyekiti wa Kijiji cha Chingumbwa, Kata ya Mbekenyela wilayani
Ruangwa, Abdallah Manjakali amesema uwepo wa mgodi huo umefungua
fursa nyingi za ajira, biashara na huduma za kijamii ambazo hapo
awali zilikuwa changamoto kubwa kwa wananchi.
“Leo wananchi
wengi wanapata kipato na maisha yameimarika. Pia kampuni imenunua
gari la wagonjwa linalowahudumia wananchi bure wakati wa dharura bila
kuchangishwa fedha yoyote,” amesema.
Manjakali ameongeza
kuwa ushirikiano uliopo kati ya mgodi na vijiji vinavyouzunguka
unapaswa kuwa mfano kwa wawekezaji wengine wa sekta ya madini, huku
akizitaka kampuni zenye leseni ambazo bado hazijaanza uzalishaji
kuharakisha uwekezaji ili wananchi waweze kunufaika na rasilimali
zilizopo katika maeneo yao.



0 Maoni