Tarehe
18 Mei, 2026, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu
Hassan, alimpokea Ikulu jijini Dar es Salaam Mkurugenzi Mkazi wa
World Bank anayemaliza muda wake, Bw. Nathan Belete, aliyefika
kumuaga Mheshimiwa Rais na kumtambulisha mrithi wake, Bw. Firas
Raad.
Katika mazungumzo yao, Bw. Belete ambaye alikuwa
akisimamia Tanzania, Malawi, Zambia na Zimbabwe, na ambaye sasa
amepandishwa kuwa Mkurugenzi wa Programu za Kikanda wa Benki ya Dunia
barani Afrika, pamoja na Bw. Raad, walizungumzia safari ya maendeleo
ya Tanzania, matarajio ya nchi kwa siku zijazo na mwendelezo wa
ushirikiano kati ya Tanzania na Benki ya Dunia.
Katika
mahojiano hayo, Bw. Belete alieleza uzoefu wake, mambo muhimu
aliyojifunza na mtazamo wake kuhusu fursa za Tanzania kwa miaka
ijayo, huku Bw. Raad akieleza matarajio yake na maeneo ya kipaumbele
anapoanza majukumu yake nchini.
BW. NATHAN BELETE, MKURUGENZI
MKAZI WA BENKI YA DUNIA ANAYEMALIZA MUDA WAKE
Unapohitimisha
kipindi chako cha miaka minne kama Mkurugenzi Mkazi wa Benki ya Dunia
nchini Tanzania, ni mafanikio au hatua gani muhimu unazozikumbuka
zaidi hata sasa unapoanza jukumu jipya la kikanda barani Afrika?
Ni
heshima kwangu kufanya kazi Tanzania, nchi nzuri yenye watu wazuri
kote Bara na Zanzibar. Hili ni jambo lenye nafasi ya kipekee katika
maisha yangu. Ninajivunia ushirikiano wetu na Serikali, wananchi na
wadau mbalimbali nchini kupitia programu kubwa inayogusa karibu sekta
zote.
Katika kipindi changu, msisitizo ulikuwa zaidi kwenye
sekta zinazogusa maendeleo ya watu, hususan elimu, afya na hifadhi ya
jamii. Programu hizi zimefanikiwa kwa kiasi kikubwa.
Tunajivunia
mchango wetu katika mageuzi ya sekta ya afya, ikiwemo bima ya afya
kwa wote, pamoja na maboresho ya elimu, hasa mitaala ya shule za
msingi na sekondari, na msukumo uliowekwa kwenye elimu ya ufundi na
stadi.
Pia ninafurahishwa na mageuzi yaliyofanyika katika
upande wa miundombinu, hasa sekta ya nishati. Katika miaka ya hivi
karibuni, tumeshuhudia Tanzania ikipiga hatua kubwa katika
upatikanaji wa nishati, pamoja na sekta ya maji na huduma za usafi wa
mazingira vijijini. Matarajio yetu ni kuona maeneo hayo yakiendelea
kukua zaidi.
Tanzania inapojiandaa kuanza utekelezaji wa Dira
ya Taifa ya Maendeleo 2050 mwezi Julai 2026, ipi ni nafasi ya Benki
ya Dunia katika kuunga mkono juhudi za kuwapa vijana na sekta binafsi
wajibu mkubwa zaidi katika mageuzi hayo?
Dira ya Taifa ya
Maendeleo 2050 ni fursa muhimu kwa Tanzania, ikichagizwa na mwelekeo
wa Serikali kwa vijana katika kukuza ajira na sekta binafsi kama
msingi imara wa kuyafikia malengo ya dira hiyo.
Kwetu sisi
Benki ya Dunia, tunaiona nafasi nzuri ya kuvutia mitaji zaidi ya
sekta binafsi kusaidia miradi mikubwa ya miundombinu ikiwemo Reli ya
SGR na maendeleo ya bandari.
Tunaamini haya yanawezekana kwa
kuwa Tanzania ni miongoni mwa nchi zenye msingi wa uchumi imara
barani Afrika na mazingira mazuri ya kuvutia uwekezaji wa sekta
binafsi.
Kwa sababu hiyo, mageuzi katika mazingira ya biashara
na uwekezaji ni muhimu. Mengi yamefanyika, lakini bado kuna nafasi
zaidi ya kurahisisha uwekezaji wa sekta binafsi nchini.
Rasilimali
za Tanzania zinaipa nchi nafasi ya kipekee, si kwa ukuaji wake pekee,
bali pia kwa maendeleo ya nchi jirani na ukanda mpana wa
Afrika.
Nafasi ya Tanzania kama kiungo cha nchi nane
zinazopakana nayo ni faida kubwa inayopaswa kuendelezwa. Kwa mtazamo
wangu, hili ni suala muhimu sana.
Namna tunavyotazama umuhimu
wa vijana na nafasi yao katika maendeleo, tunagusa moja ya malengo
makuu ya Benki ya Dunia barani Afrika, ambalo ni kutengeneza ajira
kwa vijana.
Nadhani njia hizi zinaweza kuwa msingi mzuri wa
kutengeneza ajira sambamba na mageuzi ya mitaala ya elimu ya ufundi
ambayo tayari Tanzania imeanza. Mageuzi hayo yatasaidia kuwapatia
vijana ujuzi na fursa bora zaidi za ajira. Hili ni jambo muhimu sana
kwa maendeleo ya Tanzania na bara zima la Afrika.
Zaidi ya
utajiri wa rasilimali za asili na utulivu wa kiuchumi, ni mambo gani
mengine yanayoifanya Tanzania kuwa ya kipekee katika ukanda
huu?
Tanzania ipo katika nafasi nzuri na ya kipekee ya ukuaji
wa uchumi barani Afrika. Ni nchi yenye utulivu, inayosimamia deni kwa
umakini na kutumia rasilimali zake kwa weledi. Hata hivyo, bado kuna
nafasi ya kufanya zaidi na kazi hiyo inaendelea.
Katika
majadiliano yetu kuhusu ufadhili wa Benki ya Dunia, tumeshuhudia
umakini wa Tanzania katika matumizi bora ya rasilimali
zilizopo.
Suala la msingi kwa sasa ni kupunguza utegemezi wa
miradi inayofadhiliwa na sekta ya umma na kuongeza miradi
inayofadhiliwa na sekta binafsi.
Jitihada hizi ni muhimu pia
katika kuimarisha usimamizi wa miradi, iwe ya sekta ya umma au
binafsi, na tunathamini hatua zinazochukuliwa na Serikali katika eneo
hili.
Katika kipindi ulichofanya kazi Tanzania, ni mambo gani
muhimu umejifunza utakayoyaendeleza katika jukumu lako jipya la
uongozi barani Afrika?
Mara kadhaa tumekuwa tukisema suala la
utekelezaji ni changamoto kubwa barani Afrika, lakini Tanzania, kwa
mtazamo wangu, imeonesha kuwa sekta ya umma inaweza kufanya kazi
vizuri ikijizatiti.
Tumeshuhudia baadhi ya miradi yetu
kutofanya vizuri katika baadhi ya sekta, lakini pia tumeona matokeo
makubwa katika sekta na wizara nyingine.
Niliyoyaona Tanzania
katika sekta ya nishati, maji vijijini pamoja na huduma za usafi wa
mazingira yanavutia sana. Nchi hii imeonesha kuwa utekelezaji wa
miradi katika sekta muhimu na kuleta matokeo kwa wananchi ni jambo
linalowezekana.
Ningependa kuona kasi hii ya utekelezaji
ikiendelea, kwa sababu Tanzania imeonesha kuwa hilo linawezekana pale
kunapokuwa na dhamira na utayari wa kisiasa, kiutendaji na uratibu
kati ya wadau na jamii. Hili ni moja ya masomo makubwa ninayoondoka
nayo, na ninatumaini Tanzania itaendelea kuimarisha uwezo wake wa
utekelezaji katika wizara zote.
Kwa mtazamo wako, ni katika
eneo lipi Tanzania inaweza kuweka msisitizo zaidi ili kuongeza kasi
ya maendeleo na kuhakikisha ukuaji wa uchumi unawanufaisha wananchi
wengi kwa muda mrefu?
Kuna maeneo machache ambayo, kwa mtazamo
wangu, yanahitaji kuendelea kupewa msisitizo. Kwanza, kunahitajika
umakini zaidi katika ushirikishwaji wa wananchi kwenye usanifu na
utekelezaji wa programu mbalimbali.
Pia panapaswa kuwa na
uwazi na ufanisi zaidi katika ushirikishwaji wa sekta binafsi.
Mwisho, jitihada za kuimarisha utawala bora zinapaswa kuendelezwa
katika sekta zote ili kulinda maslahi ya Taifa na wananchi kwa
ujumla.
BW. FIRAS RAAD, MKURUGENZI MKAZI MPYA WA BENKI YA
DUNIA
Kama Mkurugenzi Mkazi mpya wa Benki ya Dunia nchini
Tanzania, ni vipaumbele na fursa gani unazoziona katika hatua
inayofuata ya ushirikiano kati ya Benki ya Dunia na Tanzania?
Leo,
Benki ya Dunia imepata heshima ya kukutana na Mheshimiwa Rais wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na kujadili mtazamo pamoja na
matarajio yetu kuhusu mustakabali wa ushirikiano wetu.
Nilieleza
pia mtazamo wangu kuhusu kasi kubwa ya ukuaji wa uchumi wa Tanzania
na utulivu wa uchumi kwa ujumla. Mambo haya mawili ni msingi muhimu
wa maendeleo ya sekta binafsi tunayoyaona, na ni maeneo ambayo
tutaendelea kuyapa kipaumbele.
Kwa upande wetu sisi Benki ya
Dunia, na hili tulilieleza kwa Mheshimiwa Rais pamoja na viongozi wa
Serikali, ajenda ya ukuaji wa uchumi na ajira ni suala muhimu
sana.
Ili kufikia azma ya kupunguza umaskini kwa ufanisi,
tunahitaji si tu kukuza uchumi, bali pia kutengeneza ajira. Hili
litasaidia kufikia lengo la kupunguza umaskini na kuinua hali ya
maisha ya Watanzania wote.
Katika kufanikisha hilo, hatuna
budi kuweka mkazo katika miundombinu ya msingi ya watu na vitu,
ambayo ni elimu, hifadhi ya jamii na afya, pamoja na nishati, usafiri
na mengineyo. Hili, kwa mtazamo wangu, ni eneo muhimu sana.
Eneo
la pili ni kuimarisha mazingira wezeshi ya biashara, jambo ambalo
Tanzania imeendelea kulifanyia kazi. Tunatarajia kuendelea
kushirikiana na Serikali ya Tanzania Bara na Zanzibar katika kujenga
mazingira yatakayovutia uwekezaji unaohitajika kuendeleza kasi ya
ukuaji wa uchumi.
Na mwisho ni kutumia mtaji wa sekta binafsi
kuchochea maendeleo. Tunahitaji nguvu zaidi kuiunga mkono Tanzania
ili iweze kuvutia mtaji wa sekta binafsi katika maeneo muhimu
yanayoweza kubadili uchumi wa nchi.
Kama mnavyofahamu, nafasi
ya fedha za umma kugharamia mahitaji ya maendeleo imeendelea kuwa
finyu. Ndiyo maana ni muhimu mtaji wa sekta binafsi uingie kuongeza
nguvu katika maeneo ambayo Serikali haiwezi kuyagharamia peke
yake.
Kwa hiyo, matarajio yetu ni kuendelea kushirikiana kwa
karibu na Serikali ya Tanzania, kupanua na kuimarisha ushirikiano huu
huku tukihakikisha unaendelea kujikita katika maendeleo yanayomgusa
mwananchi moja kwa moja.
Ninatarajia kuendeleza ushirikiano
huu katika jukumu langu jipya kama Mkurugenzi wa Benki ya Dunia
ninayeisimamia si Tanzania pekee, bali pia Malawi, Zimbabwe na
Zambia.

.jpeg)

0 Maoni