Shehe wa Mkoa wa Dodoma, Mustapha Rajabu Shaaban, amewataka waumini wa dini ya Kiislamu na jamii kwa ujumla kudumisha amani na mshikamano kwa kuwa wasikivu na wenye kutii mamlaka.
Akizungumza katika ibada ya Idd al-Adha kwenye Msikiti wa Gaddafi jijini Dodoma, Shehe Shaaban alisisitiza kuwa kukosekana kwa utiifu na usikivu ndiko kunakosababisha migogoro na umwagaji wa damu katika jamii.
Katika kuelezea umuhimu wa ibada ya kuchinja iliyohitimisha mwezi wa Dhulhijjah, kiongozi huyo alikumbusha kuwa ibada hiyo chimbuko lake ni historia ya Nabii Ibrahim na mwanawe Nabii Ismail.
Alieleza kuwa kisa hicho si hadithi tu ya kawaida, bali ni fundisho kubwa la jinsi Nabii Ibrahim alivyomshirikisha mwanawe kuhusu ndoto ya kumchinja, jambo linalofundisha umuhimu wa kuheshimiana, kusikilizana na kutii amri za Mwenyezi Mungu na mamlaka husika.
Mwisho, Shehe Shaaban aliwasihi wananchi kuendeleza utamaduni wa kuheshimiana ndani ya familia na kitaifa, huku akiwataka kuheshimu viongozi, taasisi, na vyombo mbalimbali vya kijamii na kidini.
Alitolea mfano kamati na tume zinazoundwa ndani ya Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (BAKWATA), akisisitiza kuwa kuheshimu mifumo hiyo ndiko kunakojenga ustawi wa jamii.

0 Maoni