Rais wa Kenya, William Ruto, amesema nchi za Afrika Mashariki zina nafasi kubwa ya kuongeza biashara baina yao na kunufaika zaidi kiuchumi endapo zitachukua hatua madhubuti za kuimarisha ushirikiano wa kikanda.

Akilihutubia Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania jijini Dodoma Mei 5, 2026, Rais Ruto amesema biashara ya ndani ya jumuiya hiyo bado iko chini, ikikadiriwa kuwa kati ya asilimia 15 na 30, hali inayoonyesha kuwa sehemu kubwa ya biashara bado inafanyika nje ya ukanda huo.

Hata hivyo, amesema hali hiyo ni fursa kubwa kwa nchi wanachama kuongeza biashara baina yao, hatua itakayosaidia kufungua masoko mapya, kuimarisha viwanda na kuongeza ajira.

Ruto amebainisha kuwa vijana ndio nguzo kuu ya mafanikio ya ajenda hiyo, akieleza kuwa mamilioni ya vijana kutoka Kenya, Tanzania na ukanda mzima wanaingia kwenye soko la ajira kila mwaka wakiwa na vipaji, ari na ndoto kubwa.

Amesema vijana hao hawahitaji misaada bali wanahitaji fursa, na kwamba kwa kuimarisha ushirikiano wa kikanda, kuwekeza katika miundombinu ya pamoja na kupanua biashara, Afrika Mashariki inaweza kuwa kinara wa ajira, ujasiriamali na maendeleo endelevu kwa vizazi vya sasa na vijavyo.

Rais Ruto pia, amesema uhusiano kati ya Tanzania na Kenya ni wa kipekee na wa kihistoria, akisisitiza kuwa mataifa hayo mawili yameunganishwa si tu na mipaka, bali pia na watu, utamaduni na lugha.

Amesema kuwa “unaweza kuchagua rafiki, lakini jirani unapatiwa na Mungu,” akimaanisha umuhimu wa kudumisha uhusiano mwema wa ujirani kati ya nchi hizo mbili.

Ameeleza kuwa Tanzania na Kenya zinafanana katika mambo mengi, ikiwemo matumizi ya lugha ya Kiswahili pamoja na uwepo wa makabila yanayovuka mipaka ya nchi hizo, kama vile Wamaasai na Wakuria.

Ruto amesema uhusiano huo wa asili unapaswa kutumika kama msingi wa kuimarisha ushirikiano wa kiuchumi, kijamii na kisiasa kwa manufaa ya wananchi wa mataifa yote mawili.