Wananchi wameeleza kuwa wana imani kubwa na Tume ya Rais ya Kuchunguza Matukio ya Uvunjifu wa Amani yaliyotokea Oktoba 29, 2025 wakati na baada ya Uchaguzi Mkuu wa 2025, wakisema hatua hiyo ni kielelezo kuwa Tanzania inaendelea kujijengea misingi imara ya amani, utulivu na mshikamano wa kitaifa.
Akizungumza wakati wa mahojiano Jijini Dar es Salaam , Hassan Juma amesema kuundwa kwa tume hiyo kunaonyesha dhamira ya dhati ya uongozi wa nchi kusikiliza sauti za wananchi na kushughulikia changamoto kwa njia ya haki na uwazi.
Amesema kuwa Tanzania imekuwa ikijulikana kama kisiwa cha amani kwa muda mrefu, hivyo juhudi kama hizi zinasaidia kulinda sifa hiyo mbele ya mataifa mengine na kuimarisha imani ya wananchi kwa serikali yao.
Kwa upande wake, Peter John ameeleza kuwa njia ya mazungumzo na maridhiano ndiyo suluhisho la kudumu kwa migogoro ya kijamii na kisiasa, akiongeza kuwa hatua ya kuunda tume ni mwanzo mzuri wa kurejesha mshikamano.
“Tunapopeana nafasi ya kusikilizana, tunajenga taifa lenye nguvu zaidi. Tume hii inatoa fursa kwa kila mmoja kueleza yaliyomsibu na kupata haki yake ya kusikilizwa,” amesema Peter.
Naye Mwanaidi Said amesisitiza kuwa umoja wa kitaifa haujengwi kwa nguvu bali kwa kuheshimiana na kusameheana, akibainisha kuwa Watanzania wanapaswa kutumia nafasi hiyo kuponya majeraha yaliyotokana na tofauti za kisiasa.
Aliongeza kuwa wananchi wanapaswa kujitokeza kwa wingi kushirikiana na tume hiyo kwa kutoa ushahidi na maoni yao ili kusaidia kufikia ukweli na suluhisho la kudumu.
Kwa upande wake, Esther Lyimo amesema kuwa hatua hiyo inaleta matumaini mapya kwa wananchi, hasa wale walioguswa na matukio hayo, na kwamba ni ishara kuwa serikali inajali ustawi wa kila Mtanzania.
Esther ameongeza kuwa amani na utulivu ni msingi wa maendeleo ya taifa lolote, hivyo ni wajibu wa kila mwananchi kuilinda kwa kushiriki kikamilifu katika mchakato wa maridhiano.
Kwa ujumla, wananchi hao walitoa wito kwa Watanzania wote kuendelea kudumisha mshikamano, kuheshimu sheria na kushiriki katika mchakato wa kujenga taifa lenye amani, wakisisitiza kuwa umoja ndio nguzo kuu ya maendeleo endelevu.
Akizungumza wiki iliyopita Mwenyekiti wa Tume ya Kuchunguza Matukio ya Oktoba 29, Jaji Mkuu mstaafu, Mohamed Chande, amesema tume hiyo ni huru kwa asili kuanzia sheria iliyoianzisha, viapo vya wajumbe na hakuna mtu anayewaamrisha chakufanya.
Jaji Chande alifichua Tume anayoiongoza ina watu makini, ambao wanajua jambo lililotokea Oktoba 29 ni kubwa linalohitaji weledi katika kushughulikia.
#SisiNiWamoja

0 Maoni