Mchungaji Levent Marry Jackson Seganje wa Kanisa la Anglikana Tanzania, Dayosisi ya Central Tanganyika, ametoa wito kwa jamii kuthamini na kulinda amani, akisisitiza kuwa machafuko huharibu ustawi wa familia na taifa kwa ujumla.
Akizungumza baada ya ibada katika Kanisa la Mtakatifu Petro Miyuji jijini Dodoma, Mchungaji Seganje amesema familia ndio msingi wa maadili na mshikamano, na kwamba bila amani ndani ya familia ni vigumu kufikia utulivu wa jamii na maendeleo ya kijamii, kiuchumi na kiroho.
Ameongeza kuwa wazazi wanapaswa kuwa mfano bora kwa watoto kwa kuonesha upendo, uvumilivu na hekima katika kutatua changamoto za kifamilia, huku akisisitiza umuhimu wa kuepuka migogoro isiyo ya lazima na kukuza utamaduni wa kusameheana.
Aidha, ameitaka jamii kuwa mabalozi wa amani kwa kueneza upendo na mshikamano, huku akihimiza kumtanguliza Mungu katika maisha ili kujenga maadili yatakayodumisha amani ya kudumu.
Amesema amani ni msingi mkuu wa maendeleo ya taifa, na bila kuwepo kwa mshikamano ni vigumu kwa jamii yoyote kupiga hatua kiuchumi na kijamii.
Mchungaji Seganje ameendelea kusema kuwa vijana wanapaswa kulelewa katika misingi ya maadili mema ili waweze kuwa kizazi kinachothamini amani na utulivu wa taifa.
Pia amesisitiza kuwa kila mwananchi ana wajibu wa kulinda amani kwa vitendo na maneno, ili kuhakikisha taifa linaendelea kuwa salama na lenye utulivu.
Pamoja na mambo mengine, amewataka waumini na jamii kwa ujumla kuishi kwa upendo na mshikamano kama njia ya kudumisha amani ya kweli katika jamii.
#MezaYaUmoja

0 Maoni