Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), Deodatus Balile, amesikitishwa na tukio la uvamizi katika ofisi za Gazeti la Pambazuko zilizopo Kijitonyama, akilitaja kuwa ni la kinyama na linalohatarisha usalama wa waandishi wa habari nchini.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, watu wasiojulikana walivamia ofisi hizo usiku wa kuamkia Aprili 10, 2026 na kuiba baadhi ya vifaa pamoja na nyaraka muhimu za kazi.
Balile amesema TEF imesikitishwa na tukio hilo na imetoa wito kwa vyombo vya dola kufanya uchunguzi wa kina ili kubaini waliohusika na kuwachukulia hatua kali za kisheria.
Amesisitiza kuwa ni wajibu wa jamii pamoja na mamlaka za nchi kuhakikisha usalama wa waandishi wa habari na taasisi za habari unalindwa wakati wote ili kulinda uhuru wa habari.
Aidha, TEF imetoa pole kwa uongozi na wafanyakazi wa Gazeti la Pambazuko kufuatia tukio hilo, ikiahidi kusimama nao katika kuhakikisha usalama wa vyumba vya habari unaimarishwa nchini.

0 Maoni