Serikali imeendelea kusisitiza umuhimu wa kuwawezesha
Wakaguzi Wakuu wa Migodi pamoja na wachimbaji wadogo nchini ili
kuimarisha usalama kazini, kulinda mazingira na kuongeza mchango wa
sekta ya madini katika ukuaji wa uchumi wa Taifa.
Wito huo
umetolewa leo Aprili 23, 2026 wilayani Kahama, mkoani Shinyanga na
Mkurugenzi wa Huduma za Leseni wa Tume ya Madini, Mhandisi Aziza
Swedi, alipokuwa akifungua mafunzo kwa mameneja na Wakaguzi Wakuu wa
Migodi ya uchimbaji mdogo kwa niaba ya Katibu Mtendaji wa Tume ya
Madini, Mhandisi Ramadhani Lwamo.
Mafunzo hayo yanawakutanisha
washiriki kutoka mikoa ya kimadini ya Kahama, Mbogwe na Shinyanga
yakilenga kuimarisha uelewa wa kitaalam, usimamizi bora wa migodi,
uzingatiaji wa sheria na kanuni pamoja na kukuza uchimbaji salama na
endelevu.
Akizungumza wakati wa ufunguzi huo, Mhandisi Swedi
amesema Wakaguzi Wakuu wa Migodi wanapaswa kupewa ushirikiano na
mazingira wezeshi ili waweze kutekeleza majukumu yao kikamilifu,
hatua itakayosaidia kuzuia ajali migodini, kulinda afya za wachimbaji
na kuhifadhi mazingira yanayozunguka maeneo ya uchimbaji.
Amesema
mafanikio ya jitihada za Serikali katika kuwawezesha wachimbaji
wadogo yanategemea ushirikiano wa wadau wote, hususan mameneja na
wakaguzi wa migodi ambao ni nguzo muhimu katika kusimamia uzingatiaji
wa sheria, kanuni na viwango vya usalama.
“Serikali inalenga
kuhakikisha shughuli za uchimbaji zinaendelea kuchangia maendeleo ya
Taifa huku zikifanyika kwa njia salama zisizoathiri mazingira, afya
za wachimbaji na ustawi wa jamii,” amesema.
Aidha, amesema
kupitia usimamizi madhubuti, nchi inaweza kufikia azma ya Rais wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, ya
kuongeza mchango wa sekta ya madini katika Pato la Taifa kutoka
asilimia 10 ya sasa hadi asilimia 12.5 ifikapo mwaka 2030.
Ameeleza
kuwa wachimbaji wadogo tayari wanachangia takribani asilimia 40 ya
mapato yatokanayo na shughuli za madini, hali inayoonesha umuhimu wao
katika uchumi wa Taifa, huku akiwataka wamiliki wa migodi kuhakikisha
taarifa za uzalishaji na kumbukumbu muhimu zinatunzwa ipasavyo ili
Serikali ipate mapato stahiki kwa wakati.
Mhandisi Swedi pia
ameonya kuhusu athari za uchimbaji usiozingatia taratibu, akitaja
matumizi holela ya kemikali hatarishi kama zebaki na sayanaidi pamoja
na vumbi la silica kuwa chanzo cha magonjwa hatari ikiwemo silicosis,
kifua kikuu na saratani.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa
Ukaguzi wa Migodi na Mazingira kutoka Tume ya Madini, Mhandisi Hamisi
Kamando, amesema Wakaguzi Wakuu wa Migodi wanapaswa kuwasilisha
taarifa za ukaguzi mara kwa mara ili kuiwezesha Serikali kubaini
mapema vihatarishi vinavyoweza kusababisha ajali na kuchukua hatua za
kinga kwa wakati.
Amesema bado kuna changamoto katika baadhi
ya maeneo ya migodi ikiwemo ukiukwaji wa sheria, ukosefu wa
kumbukumbu sahihi za uzalishaji, ukwepaji wa kodi na utoroshaji wa
madini, hivyo mafunzo hayo yanalenga kuwajengea washiriki uwezo wa
kuwa mabalozi wa uzingatiaji wa sheria na taratibu za sekta
hiyo.
“Tunataka kuona wachimbaji wanaingia migodini salama
na kurejea majumbani mwao salama kila siku. Uhai wa binadamu una
thamani kubwa kuliko madini,” amesema Mhandisi Kamando.
Naye
Mwenyekiti wa Chama cha Wachimbaji Wadogo wa Madini Mkoa wa Shinyanga
(SHIREMA), Hamza Tandiko, amesisitiza umuhimu wa weledi kwa
wachimbaji na utoaji wa taarifa sahihi za shughuli za uchimbaji, huku
akipongeza mchango wa wakaguzi katika kupunguza ajali na madhara
migodini.



0 Maoni