Tume ya kuchunguza matukio ya uvunjifu wa amani yaliyotokea Oktoba 29, 2025, imeweka hadharani mkakati wa kundi la wanasiasa na wanaharakati uliotumika kuchochea ghasia nchini. Ripoti hiyo imebaini kuwepo kwa vichocheo vinane vilivyotumika kwa makusudi kupandikiza hasira miongoni mwa wananchi.
Akiwasilisha ripoti hiyo kwa Rais Samia
Suluhu Hassan katika Ikulu ya Magogoni leo Aprili 23, Mwenyekiti wa
tume hiyo, Jaji Mkuu Mstaafu Othman Chande, alisema baadhi ya
wanasiasa walitumia changamoto za maisha zinazowakabili wananchi kama
fursa ya kuwashawishi kushiriki ghasia kupitia kauli mbiu na matamko
mbalimbali yenye mrengo wa uasi.
Jaji Chande alitaja baadhi ya
kauli hizo kuwa ni pamoja na ‘No reform no election’, ‘Samia
must go’, na ‘Tunahakikisha nchi haisimami mpaka serikali
iondoke’. Alibainisha kuwa kauli hizi zililenga kuaminisha umma
kuwa serikali imepoteza uhalali na kwamba hakuna haja ya kufanyika
kwa uchaguzi bila mabadiliko ya mfumo.
Aidha, ripoti hiyo
imemulika matumizi ya mitandao ya kijamii kama chombo kikuu cha
kuratibu ghasia hizo. Jaji Chande alieleza kuwa wabunifu wa mada
mtandaoni walihamasisha wananchi kutoshiriki uchaguzi mkuu na kupanga
mbinu za kuhujumu mchakato mzima.
Aliongeza kuwa baadhi ya
washiriki wa ghasia walikiri kupewa simu maalumu za mkononi kwa ajili
ya kupiga picha za majeruhi, vifo, na harakati za magari ya jeshi ili
kutoa taswira potofu mtandaoni na kuibua hasira zaidi kwa
wananchi.
Mwenyekiti huyo pia alibainisha kichocheo kingine
kuwa ni wanasiasa waliokatwa majina yao katika mchakato wa kuwania
ubunge na udiwani ndani ya vyama vyao. Watu hao walitajwa kuhamasisha
ghasia hizo chinichini kwa matumaini kuwa vurugu hizo zingesaidia
kuleta mabadiliko ya mfumo utakaowabeba.
#RipotiYaTume #UkweliOkt29

0 Maoni