Rais Samia Suluhu Hassan
ametangaza mkakati wa haraka wa mambo sita yenye lengo la kuirejesha
Tanzania kwenye misingi yake ya amani, ukiwa ni muendelezo wa falsafa
yake ya 4R.
Katika hatua ya kwanza ya kusafisha kidonda cha
machafuko ya Oktoba 2025, Rais ametangaza kuunda Tume ya Maridhiano
itakayowashirikisha wadau wote muhimu nchini.
Rais
alibainisha kuwa ghasia hizo zilichelewesha mpango wake wa awali wa
maridhiano, hivyo sasa atabadili hadidu za rejea ili kuendana na
mazingira ya sasa ya kidemokrasia na kijamii, akilenga kuziba mianya
ya mgawanyiko miongoni mwa Watanzania.
Kwenye upande wa haki
na sheria, Rais ametoa amri ya kuundwa kwa chombo maalum cha
upelelezi kitakachoshughulikia viashiria vyote vya jinai vilivyotajwa
kwenye ripoti ya tume.
Chombo hicho kimepewa jukumu zito la
kuchunguza vifo vya watoto, kushughulikia madai ya miili ambayo
haijapatikana, na kufuatilia hatma ya watu wanaodaiwa kutekwa.
Hatua hii inaenda sambamba na uamuzi wa kibinadamu ambapo
serikali imejitolea kugharamia matibabu, vifaa saidizi, na viungo
bandia kwa majeruhi wote, huku ikiahidi kutoa "mkono wa faraja"
kwa wafanyabiashara wadogo waliopoteza mitaji yao na ambao hawakuwa
na bima ya kulinda biashara zao.
Aidha Rais Samia aliitaka
jamii kusimama na maneno ya Mungu, na kuwaomba viongozi wa dini na
wananchi kwa ujumla kuliombea taifa lipate uponyaji wa kiroho na
kisaikolojia.
Alisisitiza kuwa ingawa ni rahisi kubomoa nchi,
ni vigumu sana kuijenga upya, hivyo akatoa wito kwa kila Mtanzania
kulinda amani na kuepuka kushawishiwa na watu wenye nia ya kuvuruga
nchi.
Rais ameweka wazi kuwa Tanzania itaendelea kujenga
mfumo wake wa demokrasia kwa kuzingatia mila, desturi, na mchakato
wake wa ndani, huku akiwaonya watumishi wa umma kuhusu uwajibikaji,
maadili, na matumizi mabaya ya rasilimali ambayo mara nyingi ndiyo
huchochea kutoridhika kwa wananchi.
#UmojaWetuNdiyoNguvuYetu
#turidhiane

0 Maoni