Wakati
ghasia za Oktoba 2025 zikionekana kuwa na sura ya kisiasa, Tume ya
Jaji Othman Chande imebaini vyanzo vitano vya ndani vilivyotoa mpenyo
kwa matukio hayo, huku ugumu wa maisha na kero za kijamii zikichukua
nafasi kubwa. Ripoti hiyo imeainisha kuwa ghasia hizo zilichangiwa na
mchanganyiko wa malalamiko ya kisiasa, kiuchumi, na utendaji mbovu wa
baadhi ya watumishi wa umma.
Katika upande wa kisiasa, Jaji
Chande alibainisha kuwa madai ya Katiba Mpya, hitaji la demokrasia
pana katika mfumo wa vyama vingi, na malalamiko ya uboreshaji wa Tume
Huru ya Uchaguzi yalikuwa miongoni mwa vyanzo vikuu. Mashahidi
waliofika mbele ya tume hiyo walieleza kuwa kutopatiwa ufumbuzi kwa
mambo hayo kulijenga kutoridhika kwa muda mrefu miongoni mwa
wadau.
Hata hivyo, ripoti imeweka uzito mkubwa katika masuala
ya kijamii na kiuchumi. Jaji Chande alitaja ugumu wa maisha, ukosefu
wa ajira, na kukosekana kwa usawa katika fursa za kiuchumi kama
baruti iliyosubiri kiberiti. Aidha, mazingira magumu ya biashara,
utitiri wa tozo na kodi, pamoja na mfumo usio rafiki wa ukusanyaji
kodi, vilitajwa kuwaumiza wananchi wengi na kuwafanya wawe tayari
kushiriki katika machafuko.
Ripoti pia imemulika mmomonyoko wa
maadili na kushuka kwa uzalendo, huku ikibainisha kuwa kero za
rushwa, madai ya utekeji, na kupotea kwa watu vilipokosa majibu
stahiki kutoka serikalini, viliongeza chuki dhidi ya mamlaka. Jaji
Chande aliongeza kuwa utendaji mbovu wa watumishi wa ngazi za chini,
hasa katika serikali za mitaa ambao hawakusikiliza kero za wananchi,
ulichochea wananchi kuona vurugu ndiyo njia pekee ya kusikilizwa.
Ha
hivyo tume hiyo ilionya kuhusu maslahi ya mataifa ya nje. Jaji Chande
alisema mataifa mengi yanatanguliza maslahi yao katika nchi zenye
rasilimali nyingi kama Tanzania, jambo ambalo linaweza kuchangia
kuyumba kwa amani ya ndani ikiwa vyanzo vya ndani havitatatuliwa kwa
wakati na kupitia utekelezaji wa mapendekezo ya tume mbalimbali.
#RipotiYaTume #UkweliOkt29

0 Maoni